Na Prisca Libaga, Arusha
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru inatarajia Kuzindua Huduma mpya za afya kwa wananchi wake ikiwa ni Pamoja na Upasuaji kwa njia ya Matundu, Utoaji huduma ya dawa za Kansa na Uzalishaji wa hewa tiba itakayosaidia kuokoa maisha ya wananchi.
Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya rufaa ya Mkoa huo, Dkt Alex Ernest alipokuwa akitoa taarifa ya utekeleza katika robo ya pili ya mwaka wa serikali katika hospitali ya Mount Meru.
Dkt. Alex ameeleza kuwa huduma mpya ya upasuaji kwa njia ya matundu inatarajiwa kuanza kazi mwezi wa kumi mwaka 2025 ambapo itasaidia kuokoa gharama na muda wa mgonjwa kukaa hospitalini, kuongeza ufanisi wa kazi kwa watoa huduma, Pamoja na kupunguza kupunguza madhara na kubakia na kovu dogo zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji.
“Huduma hii ya upasuaji kwa njia ya matundu itaanza kutolewa mwezi wa kumi mwaka huu 2025 na itasaidia kuokoa gharama na muda wa mwananchi kukaa hospitalini, itaongeza ufanisi, na kupunguza madhara ya kubakia na kovu kubwa baada ya upasuaji”. Amesema Dkt. Alex Ernest Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mount Meru.
Aidha Ameeleza kuwa Wadau Mbalimbali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wamejenga jengo la tiba Kemia Ambalo litaanza kutoa huduma ya Matibabu ya Kansa kuanzia mwezi wa tano mwaka 2025, kwa Wananchi wa Mkoa wa Arusha na Mikoa Jirani ambapo huduma hiyo itasaidia kupata dawa na kuokoa gharama za kusafiri kwenda kutafuta huduma mbali.
Dkt. Alex amebainisha kuwa jengo hilo limejengwa na wadau wa maendeleo kutokana na faida ambazo wamezipata baada ya Mh. Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassani Kufungua Milango ya Utalii kupitia Filamu ya “The Royal Tour” ambayo imeleta matokeo makubwa kwa wananchi.
Pamoja na hayo, huduma yingine mpya zinazotarajiwa kuanza kutolewa kwa wananchi ni pamoja na upatikanaji wa majibu ya sampuli za damu baada ya kukamilika kwa jengo la Damu salama, kuanza kwa kwa huduma ya nyumbani yaani(home based care) kwa wale wananchi ambao wanahitaji huduma saidizi wakiwa nyumbani.
Pamoja na hayo Dkt. Alex Ernest amehitimisha utoaji wa taarifa ya utendaji wa miezi mitatu iliyopita kwa kuwataka wananchi kuendelea kuitumia hospitali yao kwani serikali imeendelea kufanya maboresho makubwa huku akiwahimiza kuwasilisha changamoto zozote watakazokumbana nazo wakati wa kupata huduma katika dawati la huduma kwa wateja na ikibidi hata katika ofisi yake na kwamba mtumishi yeyeto atabainika na makosa mbalimbali atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.

