Na Mwandishi wetu, Geita
KIASI cha shilingi milioni 422 cha fedha za kusaidia jamii inayozunguka kampuni (CSR) zilizotolewa na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) zitatumika kukamilisha miradi viporo ya miundombinu ya elimu na afya ya Manispaa ya Geita.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita Yefred Myenzi akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani amesema miradi hiyo utakayotekelezwa ni zahanati na nyumba za watumishi na madarasa ya shule ambayo ilianza mwaka 2018 ila ikakwama kutokana na fedha zilizotakiwa kutopatikana.
Myenzi ameeleza kwamba ipo miradi 34 inayohitaji kukamilishwa na kuwa sasa itakamilika kabla ya mwezi Mei mwaka huu wa 2025.
Amesema miradi viporo ya toka mwaka 2018/2021 sasa itakamilika kwani walikaa na GGM wakazungumza na wakaridhia watoe fedha ili kukamilisha na wameridhia kutoa shilingi milioni 422 ili manispaa waitekeleze wenyewe na ndani ya miezi mitatu iwe imekamilia.
Myenzi amesema kukamilika kwa miradi viporo kutaondoa kelel nyingi zilizoko kwa wananchi na kwa sasa GGM ipo kwenye mchakato wa kupata wakandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya CSR kwa mwaka 2024 ambapo miradi ya shilingi bilioni 5.2 itatekelezwa.
Akizungumzia hali ya elimu kwenye Manispaa hiyo Myenzi amesema bado changamoto ya vyumba vya madarasa na madawati ni kubwa kutokana na ongezeko la wanafunzi na kuwa wanapambana kutatua changamoto hiyo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani.
“Kwa upande wa shule za msingi zenye wanafunzi 78,000 tunahitaji vyumba vya madarasa 998 ambavyo kwa bajeti hatuwezi kujenga vyote kwa wakati mmoja na badala yake tutaendelea kujenga kwa awamu ili kukabiliana na changamoto hiyo,” amesema Myenzi.
“Ukweli ni kuwa tunajenga vyumba vya madarasa na kutengeneza madawati kila mwaka lakini Geita mmebarikiwa kuzaa na kuna watoto wengi na bado wanazaliwa hivyo hii changamoto kuisha sio rahisi tunaendelea kujenga zipo shule zimejaa inabidi zianzishwe nyingine ili kupokea watoto,” amesema Myenzi.
Afisa elimu sekondari Rashid Muhaya amesema kutokana na ongezeko la wanafunzi, upo upungufu mkubwa wa madarasa, viti, meza na matundu ya vyoo pamoja na upungufu wa walimu.
Muhaya amesema kuhusu walimu tayari wamepangiwa walimu wapya 42 wa masomo ya sayansi ambao watapangwa kwenye shule zenye uhitaji mkubwa.
“Mfano shule ya Nyanza ina upungufu mkubwa wa madarasa ina wanafunzi zaidi ya 2,000 inahitaji madarasa 42 yaliyopo ni 36 shule hii imevuka kiwango cha juu cha madarasa ambacho ni 1,280 wanaopaswa kutumia madarasa 321,” amesema.
Amesema kwa sasa wanatafuta eneo jingine kwa ajili ya shule mpya ili kuondokana na changamoto ya wingi wa wanafunzi kwenye shule moja na kusema hiyo siyo kwa Nyanza pekee bali kutokana na elimu bure ongezeko la wanafunzi ni kubwa.