NA DENIS MLOWE IRINGA
ZAIDI ya bilioni 18 zimetengwa kupitia mradi wa Uboreshaji Miji (TACTIC) kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa katika kata ya Kihesa na ujenzi wa barabara ya Mkimbizi Mtwivila kwa kiwango cha Lami kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Hayo yamezungumzwa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ibrahim ngwada wakati wa Kikao cha Baraza la madiwani kilichokaa hivi karibuni wakati wa Kupitisha Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ya halmashauri hiyo.
Meya Ngwada alisema kuwa katika kuboresha mji wa Iringa watakamilisha miradi mbalimbali likiwemo soko la Kihesa ambalo litakuwa kubwa kuliko soko la kisasa la Mlandege.
Alisema kuwa soko lililopo sasa la Kihesa litabomolewa na kujengwa soko la kisasa ili kukidhi utoaji wa huduma bora kwa wananchi mkoani hapa.
Alisema kuwa hadi sasa halmashauri imeshatekeleza miradi mbalimbali 18 ikiwemo kituo cha afya Mkimbizi ambacho kimeshaanza kufanya kazi, Kituo cha Afya Mkwawa kinaendelea na kazi na uwekezaji shilingi bilioni 3.5 katika hospitali ya Flerimo.
Aliongeza kuwa wamekamilisha mradi mingine kama Wodi ya watoto, karakana ya madawa, wodi za baba na mama, kituo cha afya Isiikalilo, ujenzi kituo cha Afya kata ya Kitwiru.
“* Kwa upande wa Afya hakika mama Samia katupendelea sana kwani vituo na zahanati zimejengwa kusaidia wananchi tunashukuru sana rais wetu kwa kufanikisha yote hayo ndani ya muda mfupi” Alisema
Alisema kuwa elimu miradi mbalimbali imejengwa ikiwemo ujenzi wa mabwenj, shule bora ya kisasa ya eneo la Uyole, Nduli na Kitwiru.
Meya alisema kwa upande wa barabara zitajengwa kwa kiwango cha lami za km5.11 katika kata ya Mtwivila na Mkimbizi ambapo tangazo limeshatoka la ujenzi la kutafuta wakandarasi.
Aidha halmashauri ya Manispaa ya Iringa itajenga jengo la ghorofa moja kwa ajili ya ofisi ya mkandarasi, ujenzi wa daraja kata ya Kitwiru litakalounganisha na kata ya Isakalilo ikiwa ni moja ya ahadi ya rais Samia aliyotoa kwa wananchi mkoani hapa.
Aliongeza kuwa Manispaa itajenga barabara ya mawe kama mfano kutoka shule ya Kiingereza ya Mapinduzi hadi eneo la Sunset Hotel ikiwa ni kuongeza uboreshaji wa barabara hizo ambapo eneo hilo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mahotel mbalimbali na kutaka wananchi kujitokeza kununua viwanja.
Katika bajeti hiyo maeneo mengine yatakayofaidika ni barabara ya Kondoa Wihanzi hadi Mwembetogwa na Kijificheni, barabara ya kuelekea ofisi ya mkuu wa wilaya ambapo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
“Jumla ya Mitaa 11 kunufaika na barabara za lami na vumbi na mawe, manispaa itaongeza taa za barabarani 10 ikiwemo eneo la Makanyagio na kuelekea ikulu ndogo eneo la Gangilonga.” Alisema
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARULA Mkoa wa Iringa Carol Lunyili alisema kupitia mradi wa kimkakati wa Uboreshaji miji (TACTIC) utaboresha miundombinu hasa ya barabara zilizopo katika kata za Mkimbizi Mtwivila na Kihesa kutokana na changamoto zilizopo.
Naye Diwani wa Kata ya Mtwivila Addo Gwegime amewashukuru TARULA wanazofanya na kuwaomba kuzifanyia kazi baadhi ya barabara zilizopo katika kata hiyo kwa kuwa zimekuwa zikiingizwa kwenye bajeti lakini hakuna utekelezaji.


