Na Dixon Hussein – Moshi
Katika hatua isiyo ya kawaida katika siasa za Tanzania,
diwani pekee wa upinzani katika baraza la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa
ya Moshi Frank Kagoma (Chadema) ameungana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoa pongezi kwa Mkurugenzi
wa Manispaa ya Moshi kwa usimamizi thabiti wa mapato na miradi ya maendeleo.
Mh Kagoma ambaye ni diwani wa kata ya Kiboriloni na viongozi
wa CCM wilaya ya Moshi wametoa pongezi hizo wakati wa kikao cha Baraza la
Madiwani kilichofanyika mjini Moshi, ambapo viongozi wa halmashauri hiyo
walitangaza ongezeko kubwa la mapato kutoka bilioni 41.7 hadi bilioni 53.2
katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24.
Katika kikao hicho,Mh Kagoma amekiri kuwa licha ya tofauti
za kisiasa, hawezi kupuuza ukweli kwamba usimamizi mzuri wa halmashauri umeleta
matokeo chanya kwa wananchi wa Moshi.
“Mimi ni mpinzani lakini siwezi kupinga maendeleo
yanayoonekana. Tumeona miradi ya halmashauri ikitekelezwa kwa wakati, mapato
yakiongezeka,hii ni hatua nzuri kwa wananchi,” alisema.
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Moshi wakiongozwa
na Mwenyekiti wake Faraji Swai pamoja na Madiwani wa CCM wameonyesha furaha yao
kwa ufanisi huo, wakisema kuwa halmashauri inatekeleza kwa vitendo ilani ya
chama chao kwa kuhakikisha rasilimali zinatumika ipasavyo kwa maendeleo ya
wananchi.
Mstahiki meya wa Manispaa ya Moshi Zuberi Kidumo alisisitiza
kuwa mafanikio haya ni matokeo ya mshikamano kati ya baraza la madiwani, timu
ya wataalamu wa halmashauri, na wananchi.
“Sisi tumejifunza kuwa maendeleo hayana chama.
Mkurugenzi wetu amesimamia vyema ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi,
na leo tuna bajeti inayotekelezeka kwa zaidi ya asilimia 60, kitu ambacho
hakijawahi kutokea katika miaka ya nyuma,” alisema Mwenyekiti huyo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Mwajuma Nasombe akitokwa na machozi amewashukuru
viongozi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Moshi kwa kutambua mchango ambao watendaji
wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wafanya kwa niaba ya wananchi .
Hatua hii ya mshikamano wa kisiasa imeibua mjadala mpana
kuhusu umuhimu wa kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, huku wadau
wa siasa wakisema kuwa inaweza kuwa mfano kwa halmashauri nyingine nchini.