WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametoa siku mbili kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuvunja ukuta uliozidi kwenye kiwanja namba P18618 kilichopo eneo la Kigogo jijini Dar es Salaam baada ya mmiliki wake kushindwa kuwasilisha nyaraka za uhalali wa kiwanja hicho.
Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo leo Februari 15, 2025 wakati akizungumza na wananchi wa eneo hilo ambao wamekua na mgogoro wa muda mrefu na mmiliki wa kiwanja hicho mali ya Kampuni ya Nizar Food.
“ Mtakumbuka nilikuja hapa Januari 21 mwaka huu na tukafanya mkutano wa pamoja na nyinyi wananchi na mwakilishi wa Kampuni hii, nilitoa haki ya kuwasikiliz na kuwaagiza waniletee nyaraka zinazoonesha uhalali wao wa kujiongezea kiwanja hichi lakini wameshindwa kufanya hivyo ndani ya muda niliowaagiza.
Wataalamu kupitia Kamishna wa Ardhi walipitia michoro ya eneo hili na kujiridhisha ya kwamba viwanja hivi viliongezwa kinyemela, sasa lazima tulinde maeneo yetu ya wazi. Na kwa sababu hiyo naagiza ukuta huu ubomolewe pale ulipozidi,” Amesema Mhe Ndejembi.