



Mkuu wa Mkoa w Mwanza, Said Mtanda,akizindua kamati hiyo leo, amesema itasogeza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi ili kupunguza migogoro dhidi ya Serikali na kupata suluhu ya changamoto hizo.
Amesema Kamati hiyo ya Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Sheria bila malipo itawasaidia wananchi wasio na uwezo wenye malalamiko,migogoro na kesi dhidi ya Serikali kupata fursa ya kushauriwa,kuelimishwa bure na kupata uelewa wapi wapeleke malalamiko yao.
Mtanda amesema kamati na kliniki hizo zinalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kuzifahamu haki zao na wajibu walionao katika kupata au kutafuta haki zao pia, zitasaidia kuokoa fedha nyingi za serikali zinazotokana na tozo zinazotolewa dhidi ya serikali katika mahakama na mabaraza ya kimataifa.
“Kamati na Kliniki hizo zitasikiliza na kutatua malalamiko ya kisheria yanayowakabili wananchi kutokana na ukweli kuwa wananchi wengi wao hasa maeneo ya vijijni kushindwa kumudu gharama za kufika au kupata huduma au kukosa majibu kutoka katika mamlaka husika, kliniki zitawasaidia wananchi kufahamu wapi watapata huduma za kisheria,”alisema.
Mkuu huyo wa mkoa amesema baadhi ya wananchi hawendi katika mikutano ya kisheria badala yake hukumbilia mikutano ya kisiasa kupata huruma ya viongozi ambao maamuzi yao husababisha serikali kufikishwa mahakamani.
Amesema kamati zitatoa huduma bure kwa wananchi wasio na uwezo wa kupata huduma ya mawakili ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima,ni muhimu kutumia vyombo vya kisheria badala ya kukimbilia mikutano ya kisiasa kutafuta huruma kwani kamati na kliniki ya sheria zina faida ya kupunguza migororo dhidi ya serikali na zimeundwa na wadau mbalimbali weledi wa sheria.
Mtanda amesema adhima kubwa ya kuundwa kwa kamati ni utekelezaji wa matakwa ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,ili kuwafikia wananchi walipo wenye kero nyingi wakiwemo waliodhulumiwa ardhi na wasio na uwezo wapate huduma bila malipo.
Awali Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OMMS),Neema Ringo amesema kuazishwa Kamati ya Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Sheria bila malipo kumetokana na ongezeko la idadi ya wananchi wenye nia ya kuishtaki serikali kwa sababu ya kukwazwa na huduma zinazotolewa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Amesema zaidi ya wananchi 500 kwa mwaka walionesha nia ama kusudio la kuishitaki serikali mahakamani,hivyo kuashiria kuwa watendaji wa serikali hawazingatii utawala bora wa sheria na hivyo kukiuka haki za wananchi.
“Wingi huo ulisababisha kamati hizi ziundwe ili kuwasikiliza na kupata uelewa kabla ya kuishitaki serikali.Changamoto hiyo inaashiria kuwa hatuko vizuri.Tayari Kanuni na Mwongozo umetungwa na kuzinduliwa Machi 21,2024 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,”amesema Ringo.
Aidha, amesema utafiti uliofanywa na OMMS ulibaini hakuna mfumo rasmi wa kushughulikia malalamiko ambayo hayajarasimishwa kimadai na kijinai,hivyo mwongozo huo umee utaratibu wa serikali kusikiliza na kutatua kero hizo za kisheria bila malipo.
Kwa mujibu wa Ringo kamati hizo zitasimamiwa na OMMS na zitasikiliza malalamiko ya wananchi kupitia kliniki kila mkoa hususani malalamiko dhidi ya serikali ili kuimarisha utawala bora ambapo Kamati hiyo ya Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Sheria bila malipo itakuwa endelevu.