MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es
Salaam, imeamuru kukamatwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Taifa ya
Biashara (NBC), Theobald Sabi, kwa kushindwa kutekeleza hukumu
inayoitaka benki hiyo kurudisha hati ya umiliki wa kiwanja kilichopo
Kariakoo kilichotumika kudhamini mkopo wa shilingi bilioni 3.
Jaji
Lusungu Hemed alitoa amri hiyo Jumatatu Februari 17, 2025 baada ya
kuridhia maombi ya utekelezaji kwa Mkurugenzi Mkuu wa NBC kukamatwa na
kufungwa jela akiwa mfungwa wa madai kwa kushindwa kutii huku ya
mahakama iliyotolewa takriban miaka kumi iliyopita.
“Mkurugenzi
Mkuu wa Mdaiwa wa Kwanza (Benki ya Taifa ya Biashara) akamatwe na
kufikishwa mahakamani hapa Machi 11, 2025 saa 9.00 asubuhi kwa ajili ya
mchakato wa kuwekwa kizuizini,” Jaji hemed alisema katika amri yake ya
Februari 17, 2025.
Mmiliki wa kiwanja hicho, Ramadhani Massudi na
Family LTD alifungua maombi ya kukazia hukumu baada ya kushinda kesi ya
ardhi, ambayo hukumu yake ilitolewa na Jaji Sophia Wambura, ambaye sasa
amestaafu, Julai 24, 2015, akiiagiza benki hiyo kurudisha hati ya
kiwanja hicho kwa mmiliki.
Maombi hayo yalisikilizwa na Naibu
Msajili Wanjah Hamza na kubaini kwamba kwa kuwa amri hiyo ni ya 2015,
mahakama iliona kuwa Benki na Mkopaji Mkuu, Haji Associates (T) Ltd,
wameshindwa kuonyesha sababu za kutosha kwa nini utekelezaji wa hukumu
hiyo usiendelee.
Mnamo Februari 23, 2024, aliiamuru Benki hiyo
kukabidhi mara moja hati ya kiwanja kilichopo Mtaa wa Ungoni ndani ya
Manispaa ya Ilala kwa mmiliki, Ramadhani Massudi and Family LTD, mbele
ya Naibu Msajili na Haji Associates (T) LTD imlipe Tsh 150m/- kama
fidia.
Kwa vile mwenye hati hiyo hakuwa ametaja ni namna gani
usaidizi wa mahakama ulihitajika kukazia hukumu hiyo ya mwaka 2015,
mahakama ilimwagiza atafute ni njia ipi ingekuwa bora zaidi na
kuifahamisha ipasavyo kwa mujibu wa sheria.
Kwa kuzingatia
maagizo ya mahakama, Oktoba 30, 2024, mwenye hati hiyo kupitiaWakili
Avodius Lutabingwa, aliwasilisha maombi ya kukazia hukunu hiyo, akiomba
Mkurugenzi Mkuu wa NBC, Theobald Sabi, akamatwe na kufungwa kama mfungwa
wa madai baada ya kushindwa kurudisha hati yake.
Pande zote
mbili zilifika mbele ya Jaji Hemed mnamo Desemba 2, 2024 ambapo Wakili
Mariam Ismail, wa NBC, aliomba mteja wake aonyeshe sababu kwa nini
asikamatwe kwa njia ya hati ya kiapo. Wakili Lutabingwa hakupinga ombi
hilo.
Jaji Hemed aliiamuru Benki hiyo kuwasilisha hati ya kiapo
hiyo Desemba 16, 2024 na mwenye tuzo akaelekezwa kuwasilisha hati ya
kiapo kinzani Januari 2, 2025. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 17,
2025 kwa ajili ya kusikilizwa.
Kesi hiyo ilipoitwa kusikilizwa
Februari 17, 2025, Wakili Hamis Nkya na Africa Mazoea walifika mbele ya
Jaji Hemed kwa naiba benki hiyo, huku Wakili Lutabingwa akimwakilisha
mwenye tuzo na kuieleza mahakama kuwa hajakabidhiwa hati ya kiapo ambayo
ilikuwa iwasilishwe na benki hiyo.
Wakili Nkya alisimama na
kuieleza mahakama kuwa wameamua kutowasilisha hati ya kiapo ili
kuonyesha ni kwa nini Mkurugenzi Mkuu wa NBC asikamatwe na kupelekwa
gerezani kama mfungwa wa madai na kuomba aruhusiwe kufanya hivyo kwa
njia ya mdomo.
Katika amri yake, Jaji Hemed alieleza kuwa mdaiwa
analazimika kufuata utaratibu uliochaguliwa na mahakama na iwapo
atashindwa kufanya hivyo hadi tarehe iliyopangwa na mahakama,
itachukuliwa kuwa hana sababu ya kuonyesha na kujitetea.
“Katika
maombi ya sasa, mdaiwa ameshindwa kuzingatia amri ya mahakama ya
kuonyesha sababu kwa njia ya hati ya kiapo. Katika hali ya kesi hii,
sina njia nyingine zaidi ya kukubali maombi haya,” Jaji alisema akaamua.
Mwaka
1998, Ramadhani Massudi alitoa hati yake ya kiwanja kilichoko Mtaa wa
Ungoni, ili kumwezesha Haji Associates (T) LTD kupata mkopo wa kiasi cha
bilioni 3 kutoka NBC. Rehani hiyo ilikuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mwishoni
mwa mwaka huo mmoja, hati hiyo haikurudishwa. Massudi alimfuata Haji
Associates kuuliza kulikoni, lakini akahakikishiwa kwamba hati hiyo
ingerudishwa. Hata hivyo, hati hiyo haikurejeshwa kwa madai ya benki
kuwa mkopo uliochukuliwa haukurejeshwa.