NA DENIS MLOWE, IRINGA
MSANII wa Muziki wa aina ya Bongo Fleva kutoka mkoani Iringa, Ezra Msiliova Maarufu kama EzeNice akiongozana na baadhi ya wasanii mbalimbali mkoani hapa wametembelea kituo cha kulelea yatima na wanaoishi katika mazingira Magumu cha Amani Center na Kutoa misaada mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kusambaza upendo wa watoto hao.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi msaaada huo ikiwa ni kusheherekea siku ya kuzaliwa kwa mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa Mnec Salim Abri (Asas) ambaye amefadhili kwa asilimia kubwa msaada huo Eze Nice alisema kuwa watu wote wajifunze kuwatembelea watoto yatima kwa lengo la kuwafariji na kuwaonyesha upendo ambao wamekosa kutoka kwa wazazi wao.
Alisema kuwa watoto hao ni wetu tukiwaacha katika mazingira hayo nani atawalea hivyo ni jukumu la jamii kuwaona na kuwapa mahitaji ambayo wanahitaji kuliko kuwaaachia vituo hivyo pekee na serikali kulea watoto hao.
Alisema kuwa kupitia Mnec Salim Asas waliweza kutoa misaada mbalimbali ya kibinadamu vyenye thamani ya zaidi ya milioni 1.5 kwa kituo hicho chenye watoto 82 ikiwa wa kike 43 na wa kiume 39.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo Mkuu wa Kituo hicho, Elizabeth Mwakabanga alisema kuwa kituo hicho kinapokea watoto kutoka maeneo mbalimbali kuanzia umri wa miaka 4 hadi 10 na kuwalea hadi kufikia malengo yao ya kielimu kwa kupitia misaada ya watu wa Ujerumani na kanisa la kikatoliki mkoani hapa.
Alisema kuwa lengo la kuanzishwa kituo hicho ni kuondoa mtazamo wa kidini kwa kupokea watoto wa dini zote ambapo kilianza na watoto 13 hadi sasa kufikia watoto 82.
Aidha kituo hicho kinatoa hifadhi kwa watoto wanalioathirika na ukatili na kuwapa huduma za kisheria wanazokosa watoto hao.
Mwakabanga alisema kuwa licha ya kuwepo kwa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi, madawa, upungufu wa vifaa vya michezo, vifaa mbalimbali vya shule ikiwemo sare za shule, viatu, magodoro nk.
Ametoa wito kwa jamii kuweza kusaidia watoto yatima walioko katika maeneo mbalimbali nchini kwani Baraka kwa mwenyezi Mungu kwa watoaji.