DENIS MLOWE, IRINGA
ZAIDI ya washiriki 230 kutoka kada za afya, sekondari , watumishi ofisi ya Mkurugenzi na watendaji kata wamepata mafunzo ya mfumo mpya wa manunuzi umma (NeST) ambao ni mbadala wa mfumo wa awali wa Tanzania National e Procurement System yaani (TANePS) katika ngazi ya msingi yanayofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Akizungumza wakati wa uznduzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Charles Mwakalila alisema kuwa watumishi hao kuzingatia mafunzo hayo yenye tija katika manunuzi ya umma na kufanya majaribio zaidi kuweza kuuelewa mfumo huo kwani lengo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuleta uwazi.
Alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa watumishi hao kwani imekuwa ni mfumo wenye ubora ingawa imekuwa changamoto kwa wanaofanyia kazi ambao ni watumishi hali hivyo mafunzo haya yatawasaidia katika kuboresha utendaji kazi wao na kuondokana na changamoto mbalimbali.
“Mnatakiwa kuwa na umakini mkubwa sana katika mafunzo haya kwani uelewa na utekelezaji wa mfumo huu ni matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kuwa na matumizi mazuri na sahihi ya fedha za umma katika ununuzi wa vifaa na huduma na hatimaye kuwaletea Watanzania maendeleo yaliyokusudiwa mama Samia Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema
Mwakalila alisema kuwa ofisi za serikali katika upande wa manunuzi wanatakiwa kutumia mfumo huo wa NeST kwani kutotumia itasababisha kufungwa jela au malipo ya milioni 10 kitu ambacho kila mmoja anatakiwa kutumia mfumo huo wa serikali katika manunuzi kuepuka changamoto pindi asipotumia mfumo huo.
Mafunzo hayo yanatolewa kwa kada hizo na mkufunzi kutoka Mamlaka ya Umma ofisi ya Manunuzi kanda ya Nyanda za Juu kusini, Antony Masam ambaye alishilikiana na Daniel Kimaro.
Antony Masam ambaye ni miongoni mwa wakufunzi wa mafunzo hayo, alisema mfumo wa NeST ni Mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma umelenga kutatua changamoto za mfumo wa awali wa Taneps na kuongeza kuwa ni mfumo bora na salama kwani umetengenezwa na Watanzania, pia ni mfumo rafiki na rahisi kwa watumishi ambao utasaidia kudhibiti rasilimali za Serikali na utazuia mianya yote ya upendeleo na rushwa katika mchakato wa manunuzi, kuharakisha utendaji na kuongeza uwazi.
Naye Afisa Manunuzi Manispaa ya Iringa, Dismas Mwakasambwe alisema kuwa mafunzo hayo yatatatolewa kwa Idara na Vitengo mbalimbali vya manispaa na katika mafunzo hayo washiriki watapitishwa katika maeneo mbalimbali ya Mfumo ili waweze kuwa na uelewa wa kutosha kabla ya kuanza matumizi hayo ambayo yamekuwa na changamoto kwa watumiaji wenyewe.