Raia wa Marekani anayeshtumiwa kujaribu kusafirisha Cocaine kutoka Alabama, Marekani, hadi Saudi Arabia, anapokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi chini ya ulinzi wa polisi, baada ya kupata matatizo makubwa ya kiafya.
Mshukiwa huyo, Jarod Tyler Roberts, alifikishwa hospitalini Jumapili, Februari 16, 2025, na rafiki yake baada ya kuonyesha dalili za madhara makali ya dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa DCI, mshukiwa alilazwa kwa uchunguzi wa kimatibabu, ambapo madaktari walibaini uwepo wa dawa hizo mwilini mwake.
Mnamo siku ya Jumanne, Februari 18, 2025, daktari aliyekuwa akimhudumia Roberts aliwaarifu maafisa wa kitengo cha kupambana na mihadarati cha DCI, ambao walifika hospitalini kushuhudia upasuaji wa endoskopi uliofanywa kwa mshukiwa.
Wakati wa upasuaji huo, vidonge vitatu vya Cocaine vilivyofichwa kwenye njia ya haja kubwa ya mshukiwa vilipatikana, na vilipimwa kuthibitisha kuwa ni Cocaine yenye uzito wa gramu 57.98. Ushahidi huo ulichukuliwa na kuthibitishwa rasmi na maafisa wa DCI.
Aidha, daktari alithibitisha uwepo wa kidonge kingine cha Cocaine kilichokwama kwenye utumbo mdogo wa mshukiwa, na juhudi za kimatibabu zinaendelea ili kukiondoa kwa usalama wake.
Uchunguzi wa maafisa wa DCI umebaini kuwa Roberts alikuwa akiishi kwa muda mfupi katika Airbnb iliyoko eneo la Westlands, Nairobi.
Mshukiwa alikuwa amepanga kusafiri kwa ndege ya Ethiopian Airlines saa 12 jioni siku aliyougua, kupitia Addis Ababa kuelekea Saudi Arabia.
The post Anayeshtumiwa kujaribu kusafirisha Cocaine kwenye njia ya haja kubwa hoi hospitali first appeared on Millard Ayo.