Makamu Mwenyeti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na
Sheria Mhe. Florent Kyombo akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea na
kukagua Taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar leo Februari 19, 2025.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza akizungumza
wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria
kutembelea na kukagua Taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar leo Februari 19, 2025.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja
akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala,
Katiba na Sheria kutembelea na kukagua Taasisi za Muungano zilizopo
Zanzibar leo Februari 19, 2025.
Wajumbe wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakiwa
katika picha ya pamoja wakati wa kutembelea na kukagua Taasisi za
Muungano zilizopo Zanzibar leo Februari 19, 2025.
……..
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imetoa pongezi
kwa Serikali kwa kutekeleza na kusimamia miradi ya Muungano Zanzibar na
hivyo kuleta manufaa kwa wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Florent
Kyombo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua Taasisi za Muungano
zilizopo Zanzibar leo Februari 19, 2025.
Miongoni mwa Taasisi zilizotembelewa na Kamati ni pamja na Tume ya Vyuo
Vikuu Tanzania (TCU), Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Tume ya Pamoja
ya Fedha (JFC).
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kyombo
amesema miradi hii ni matunda ya uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Katika mradi wa Mbweni katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Karume
(KIST) uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi, Makamu Mwenyekiti amesema Kamati
imeridhishwa na mradi huo.
“Tuwapongeze na kuwashukuru viongozi wakuu wa Serikali zote mbili kwani
kupitia miradi hii, viongozi hawa wamefanya mapinduzi makubwa katika
ujenzi wa miundmbinu na huduma za jamii na ubora wake unaonedkana,”
amesema.
Mhe. Kyombo ambaye pia ni Mbunge wa Nkenge amewataka wananchi
kuendelea kuwapa ushirikiano Viongozi hao wakuu na Serikali kwa ujumla ili
miradi hiyo iwafikie na kutoa huduma stahiki.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza
Khamis amesema Ofisi hiyo inatarajia kujenga jengo mahsusi litkalojumuisha
taasisi zote za Muungano upande wa Zanzibar.
Amesema pamoja na mpango tayari Serikali ya Jamhuri ya Muungano
imekwishajenga majengo ya taasisi zake ambayo yanaendelea kutoa huduma kwa wananchi.
“Niwaambie tu Serikali zote mbili zinatekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo ili kusogeza karibu huduma kwa wananchi na hivyo waweze
kufurahia matunda ya Muungano,” amesisitiza Mhe. Khamis.
Pamoja na maeneo hayo pia Kamati ilipata wasaa wa kutembelea na kukagua
kiwanja ambacho kutajengwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itayojengwa
Zanzibar.
Ziara hiyo pamoja na viongozi mbalimbali iliwashirikisha Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja, Naibu Katibu Mkuu (Muungano)
Bw. Abdallah Hassan Mitawi na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais
na Taasisi hizo.
Hii ni ziara ya kwanza kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na
Sheria kufanya ziara katika Taasisi za Muungano zilizopo katika upande wa
Zanzibar.