NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Wilaya ya Iringa Kheri James awahimiza wazazi kufuatilia maendeleo ya kielimu ya watoto wao pindi wanapokuwa shuleni na nyumbani kubaini uwezo na mapungufu yao kwa kushirikiana na walimu.
Akizungumza wakati wa kikao cha kutathimini mitihani ya kidato cha pili, nne na sita kwa mwaka 2024 Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, ametoa wito huo kwa wazazi na walezi kuanzisha tabia ya kufuatilia maendeleo ya kielimu ya watoto wao shuleni ili kuboresha matokeo yao kuwa ushiriki wa wazazi ni jambo muhimu katika mafanikio ya wanafunzi.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu wa shule za sekondari za umma na binafsi, waratibu wa elimu wa kata, na wadau wengine wa elimu kutoka Halmashauri ya Jiji la Iringa.
James alisema kuwa kadri unavyojizatiti katika kumuwezesha mtoto wako kielimu, ndivyo matokeo bora utakavyoyapata na endapo utajizatiti kidogo, matokeo nayo yatakuwa madogo, kwa mwanao na upande wa shule wakiwekeza katika udogo wa masomo na ufaulu utakuwa mdogo.
Aliongeza kuwa baadhi ya wazazi, wanapowaacha watoto wao shuleni, hawafuati maendeleo yao ya kielimu, na kuacha jukumu hilo kwa walimu pekee wajue kuwa maendeleo ya mwanafunzi ni jukumu la pamoja kati ya mzazi, mwalimu, na mwanafunzi.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Sekondari wa Manispaa ya Iringa, Tupe Kayinga, alisema kuwa kikao kama hicho kilifanyika mwaka jana, na kikao cha mwaka huu kilijikita katika kutathmini mikakati iliyotekelezwa ili kuboresha ufaulu.
“Ningependa kumpongeza Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nduli kwa kupunguza idadi ya wanafunzi waliopata sifuri kutoka 47 mwaka 2023 hadi mmoja tu mwaka 2024. Huu ni mafanikio makubwa, hasa ukizingatia changamoto zinazowakumba wanafunzi wanaotembea kilomita 26 kwenda na kurudi shuleni kila siku,” alisema Kayinga.
Alimtaja pia Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mawelewele kwa kuondoa kabisa alama za sifuri katika matokeo ya mwaka huu miongoni mwa shule za umma, huku Shule ya Sekondari ya Mtwivila ikionyesha mafanikio ya kudumu kwa kuboresha zaidi kila mwaka tangu 2022 hadi 2024.
Kayinga alisisitiza kuwa matokeo ya mwaka 2023 yalikuwa ya kutisha, ambapo wanafunzi 441 wa Kidato cha Nne walipata sifuri, na wanafunzi 326 wa Kidato cha Pili walipata alama hiyo hiyo. Hata hivyo, alionyesha kuridhishwa na juhudi zilizofanywa na halmashauri katika kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi waliofaulu.



