Dar es Salaam, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inatarajia kusherehekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975 kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazoakisi majukumu yake. Moja ya shughuli kubwa ni kampeni maalum iliyopewa jina la “Kitabu Kimoja kwa Mwanafunzi Mmoja”, yenye lengo la kuhakikisha kila mwanafunzi anapata kitabu cha kiada, hatua inayolenga kuboresha elimu nchini.
Katika kampeni hii, TET inashirikiana na wadau wa elimu, mashirika binafsi, taasisi za serikali na wananchi kwa ujumla kuchangia upatikanaji wa vitabu kwa wanafunzi wa elimu ya awali, shule za msingi na sekondari kote Tanzania Bara na Zanzibar.
Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho, TET imeandaa Matembezi ya Hisani ya Kilomita 5 yatakayofanyika tarehe 7 Machi, 2025, yakianza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (eneo la Maktaba Mpya), kupitia Chuo cha Maji, Mlimani City, Mwenge na kumalizikia katika Ofisi za TET Makao Makuu.
Matembezi hayo yatatanguliwa na uzinduzi rasmi wa sherehe za miaka 50 ya TET, ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TET, matembezi yataanza saa 12:00 alfajiri na kuhitimishwa saa 2:00 asubuhi, kisha hafla rasmi ya uzinduzi itafanyika katika viwanja vya TET kuanzia saa 3:00 asubuhi.
Katika kuhakikisha kampeni ya “Kitabu Kimoja kwa Mwanafunzi Mmoja” inafanikiwa, TET inawaalika wadau wote kushiriki kwa kuchangia kupitia njia mbalimbali.
Kwa wale wanaotaka kushiriki matembezi, ada ya usajili ni TSH. 50,000 kwa fulana na TSH. 150,000 kwa tracksuit. Fedha hizi zitatumika moja kwa moja kwa uchapaji na usambazaji wa vitabu vya kiada.
Aidha, wale wanaotaka kuchangia moja kwa moja wanaweza kutumia namba ya malipo ya serikali: 994040118259. Kampeni hii ni endelevu, na michango itaendelea kupokelewa hadi kilele cha maadhimisho mwezi Juni 2025.
Kwa mujibu wa TET, wadau wanahimizwa kufuatilia taarifa zaidi kuhusu kampeni kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii: X (Twitter): @taasisiyaelimutanzania, Instagram: @taasisiyaelimutanzania na Facebook: @taasisiyaelimutanzania
Kwa kushirikiana, Tanzania inaweza kufanikisha lengo la kuhakikisha kila mwanafunzi anapata kitabu chake kwa uwiano wa 1:1, hatua itakayoboresha viwango vya elimu nchini.