Serikali ya Tanzania imezishauri nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwekeza zaidi katika sayansi, teknolojia, utafiti na maendeleo (R&D) ili kuhakikisha sekta ya viwanda vya ulinzi inakua kwa kasi sambamba na maendeleo ya kiteknolojia duniani.
Akizungumza Februari 25, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Maofisa Wakuu wa Vituo vya Viwanda vya Kijeshi vya EAC, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, amesisitiza kuwa maendeleo ya sekta hiyo yanategemea uwezo wa mataifa wanachama kujitegemea kiteknolojia badala ya kutegemea masoko ya mbali.
“Teknolojia inabadilika kwa kasi sana, hivyo ni muhimu nasi kwenda na kasi hiyo ili tusiendelee kuzalisha vifaa vilivyopitwa na wakati. Viwanda vyetu vya ulinzi vinapaswa kutumia teknolojia za kisasa ili kuboresha uzalishaji na kuongeza tija,” alisema Sillo.
Mkutano huo umejikita katika kutathmini hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi ya awali, kujadili miundombinu inayoweza kushirikishwa kati ya nchi wanachama, na kupokea ripoti ya Kundi la Wataalamu wa Mashirika Mbalimbali (MEWG) lililokutana Kampala, Uganda.
Aidha, mkutano huo unatoa jukwaa kwa washiriki kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu teknolojia mpya za kijeshi, huku ukihamasisha ushirikiano wa kiteknolojia na upanuzi wa masoko ya bidhaa za ulinzi ndani ya jumuiya.
Sillo alisisitiza kuwa ushirikiano wa ulinzi ndani ya EAC ni fursa muhimu kwa mataifa wanachama kuimarisha viwanda vya ulinzi kwa lengo la kujitegemea, akibainisha kuwa sekta hiyo inapaswa kuwa sehemu ya mipango ya maendeleo ya muda mrefu kwa nchi za ukanda huo.
Mkutano huo wa siku mbili unajumuisha maonyesho ya viwanda vya ulinzi vya Tanzania, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa mapendekezo ya mkutano wa awali ili kuimarisha ushirikiano wa sekta ya ulinzi katika kanda.