
Mhe. Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi akimshuhudia Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti wakati akila kiapo cha kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Maafisa wa Mahakama Mkoa wa Pwani.
Mhe.Jaji Salma Maghimbi akizungumza kwenye hafla ya kuwaapisha Wajumbe wa Kamati ya Maadili na Maafisa wa Mahakama Mkoa wa Pwani iliyofanyika leo Februari 25 Kibaha.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Salma Maghimbi na Naibu Katibu wa Tume(Maadili na Nidhamu) Bi.Alesia Alex Mbuya
Mahakimu wa Mahakama za Wilaya Mkoa wa Pwani wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mhe.Jaji Mfawidhi Salma Magimbi
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani alipomuwakilisha na kufungua mafunzo hayo ya siku moja.
Na Khadija Kalili Michuzi TV
JAJI Mfawidhi Mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi ametoa wito kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama Mkoa wa Pwani kuishi kiapo chao walichoapa leo tarehe 25 Februari 2025.
“Nawasisitiza mkaishi viapo vyenu mlivyo apa pia nawashukuru kwa utayari wenu wa kuitikia kuwa kwenye Kamati hii” amesema Jaji Mfawidhi Maghimbi
Amesema kuwa Wajumbe wanapaswa kuwa na hofu ya Mungu kwa sababu kazi wanayokwenda kuifanya inahusiana na maisha ya watu.
“Tuko katika nguzo ya tatu ya mhimili wa nchi, hizo kamati zimeanzishwa kwa lengo la kumsaidia mwananchi mwenye malalamiko yake ama kutoridhishwa na maamuzi ajue wapi mahali sahihi pa kupeleka malalamiko yake.
Kamati ya Mkoa ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama inaundwa na Mkuu wa Mkoa husika ambaye atakuwa Mwenyekiti, Hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa na Wajumbe wengine wawili watakao teuliwa na Mkuu wa Mkoa kutoka miongoni mwa watu mashuhuri katika Mkoa , ambao wana uadilifu wa hali ya juu, walio na ufahamu na uwezo ambao ni muhimu katika kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wenye ufanisi wa majukumu ya Kamati pamoja na Maafisa wawili wa Mahakama watakaoteuliwa na Jaji Mfawidhi
Aidha Katibu wa Kamati hiyo atakuwa Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi katika Mikoa yenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na katika Mikoa ambayo haina Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Serikali Katibu atakuwa Katibu Tawala wa Mkoa.
“Majukumu ya Kamati ni kupokea na kuchunguza malalamiko yaliyowasilishwa na wajumbe wa umma kuhusiana na Mahakimu wa Wilaya au Mahakimu Wakaazi katika Mkoa husika na Kisha kuwasilisha ripoti Tume” amesema Jaji Mawidhi Maghimbi.
Amesema kuwa Kamati itatakiwa kufanya uchunguzi wa mwenendo wa Mahakimu wa Wilaya au Mahakimu Wakaazi kwa kuzingatia maelekezo ya Jaji Mfawidhi na kutoa ripoti kwake au kuchukua hatua muafaka kulingana na Sheria.
“Kutekeleza majukumu mengine kadiri ambavyo Jaji Mkuu anaweza kwa maandishi ya mkono wake kuelekeza kwa Mwenyekiti” amesema Jaji Mfawidhi Maghimbi.