Serikali ya Mkoa wa Mara imeunda kamati maalum ili kutafuta suluhisho la kudumu kwa mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa Kijiji cha Korotambe, Kata ya Mwema, na Kijiji cha Nyabichune, Kata ya Regicheri, wilayani Tarime.
Mgogoro huo, ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 30, umeendelea kusababisha mapigano ya mara kwa mara, yakiwemo matukio ya hivi karibuni ambapo watu watatu walijeruhiwa kwa kukatwa mapanga na ng’ombe kadhaa kujeruhiwa kati ya Februari 6 na 18, 2025.
Kamati hiyo, ambayo inaanza kazi yake rasmi leo Jumanne, Februari 25, 2025, imepewa muda wa wiki mbili kutekeleza majukumu yake. Inajumuisha wataalamu wa ardhi, wazee wa mila, na wazee mashuhuri, wenye jukumu la kutambua na kubainisha wamiliki wa ardhi katika eneo lenye mgogoro.
Majukumu mengine ya kamati hiyo ni: Kutambua mpaka wa eneo husika kwa mujibu wa ramani ya Wizara ya Ardhi.
Kutathmini mpaka unaojulikana kama Ingram, uliowekwa wakati wa utawala wa Kijerumani kabla ya Tanzania kupata uhuru.
Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo baada ya kutembelea eneo lenye mgogoro, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, amesema lengo la serikali ni kupata suluhisho la kudumu, si kuongeza uhasama.
“Nyie hapa ni ndugu, tofauti yenu ni kwamba wengine ni wa ukoo wa Wakira na wengine ni kutoka ukoo wa Wanchari. Ni jambo la kusikitisha kuona watu wa kabila moja wakipigana na kuuana kwa sababu ya ardhi,” amesema Mtambi.
Ameongeza kuwa serikali haina mpango wa kuchukua ardhi ya mtu yeyote, bali inataka kuona ardhi inatumika kwa maendeleo na kwa amani.
“Umefika wakati sasa wakazi wa Tarime na Mkoa wa Mara kuachana na tabia ya kukatana mapanga kila wanapotofautiana. Hakuna sifa ya kuua mtu, na hakuna utajiri unaopatikana kwenye ardhi iliyomwaga damu. Badilikeni ndugu zangu, tafuteni majibu ya changamoto zenu kwa njia sahihi,” amesisitiza Mtambi.
Ametoa onyo kali kwa watu wanaochochea mgogoro huo, akiwemo baadhi ya wanasiasa, na kusisitiza kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote anayesababisha vurugu, vifo, na majeruhi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele, amesema baada ya mapigano ya Februari 6 hadi 18, alifanya mkutano na wakazi wa eneo hilo ili kurejesha utulivu.
“Tulibaini kuwa kuna mkanganyiko wa mpaka pamoja na hati tatu za umiliki zenye utata. Tayari hatua zimechukuliwa ili kubaini ukweli, na shughuli zote za kilimo katika eneo hilo zimesitishwa hadi uchunguzi utakapokamilika,” amesema Gowele.
Baadhi ya wakazi wa Nyabichune na Korotambe wamesema wanataka mgogoro huo umalizike ili waweze kuendelea na maisha yao kwa amani.
“Shida hapa ni watu kupindisha ukweli kwa maslahi yao. Tunamshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuingilia kati, tunaamini sasa hili jambo litafika mwisho,” amesema Chango William.
Kwa upande wake, Makabe Mtatiro, mkazi wa eneo hilo, amesema mgogoro huo umewafanya wengi kuishi katika umaskini kwa sababu kila mapigano yanapoibuka, mazao yao hufyekwa mashambani na mifugo yao huchinjwa au kuchomwa moto.
“Watu wengi wameuawa kwa kukatwa mapanga au kuchomwa mishale. Tumechoka na hali hii, tunaiomba kamati iliyoundwa ifanye kazi haraka ili tupate suluhisho la kudumu,” amesema Mtatiro.