Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya mifugo kwa kuanzisha mradi wa utafiti wa NANO COMM, unaolenga kutengeneza tiba mbadala ya homa ya kiwele kwa wanyama wanaotoa maziwa. Utafiti huu unalenga kutatua changamoto sugu inayowakabili wafugaji, hususan katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Arusha, na Tanga.
Prof. Gaymary Bakari, Mhadhiri wa SUA na Mtafiti Kiongozi wa mradi, amesema kuwa utafiti huu ni sehemu ya juhudi za chuo hicho katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakumba wafugaji kupitia sayansi na tafiti.
“Tumebaini kuwa homa ya kiwele imekuwa tatizo sugu kwa wafugaji wa wanyama wa maziwa, ambapo wengi wao wanakosa tiba sahihi au wanatumia gharama kubwa kutibu mifugo yao,” amesema Prof. Bakari.
Ameeleza kuwa matarajio ya mradi huu ni kuleta suluhisho la moja kwa moja kwa wafugaji kwa kuongeza uzalishaji wa maziwa, kupunguza gharama za matibabu, na kuimarisha uchumi wa wafugaji.
Kwa miaka mingi, SUA imekuwa kinara wa tafiti mbalimbali zinazolenga kuboresha afya ya mifugo na kuongeza uzalishaji wa mazao yake.
Aidha, Prof. Bakari ametoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano wa karibu ili kufanikisha malengo ya mradi huo. Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya SUA, wafugaji, na wadau wa sekta ya mifugo ni muhimu kuhakikisha tiba zinazopatikana zinakuwa sahihi na zinatatua changamoto ya homa ya kiwele kwa ufanisi.
“Tutahitaji msaada wa wafugaji na jamii kwa ujumla ili kupata suluhisho bora litakalosaidia sekta hii kubwa na muhimu,” amesema Prof. Bakari.
Katika mradi huo, Ezekia Mbawa na Lisa Kisanga, wanafunzi wa Shahada ya Uzamili SUA, wanashiriki kama watafiti washiriki. Wameeleza kuwa mbali na kushiriki katika utafiti, mradi huo umewapa fursa ya kusoma shahada zao za uzamili, huku wakipata ujuzi wa kina kuhusu tiba za mifugo na tafiti za kimataifa.
“Tunaamini kuwa kupitia utafiti huu, SUA itaendelea kuwa chombo muhimu cha mabadiliko chanya katika sekta ya mifugo nchini,” amesema Mbawa.