Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA. Anthony Kasore, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 3,2025 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA. Anthony Kasore, ameeleza kuwa katika juhudi za kutatua changamoto ya ajira, VETA inajitahidi kuzalisha wahitimu wengi wenye ujuzi unaohitajika, na hivyo kuongeza idadi ya mafundi saidizi kwa kila mafundi watano, kama ilivyoainishwa katika tafiti za kitaifa.
Akizungumza leo Machi 3,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita CPA Kasore amesema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi stadi.
CPA Kasore amesema kuwa VETA ina jukumu kubwa la kutoa elimu ya ufundi stadi inayokidhi mahitaji ya soko la ajira nchini, na kuwawezesha Watanzania kupata fursa za ajira na kwamba kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Serikali mwaka 2023, asilimia 67.7 ya wahitimu wa VETA wameajirika.
Rais Samia Apaisha Mafunzo ya Ufundi Stadi
Kasore amesisitiza kuwa mafanikio haya yanadhihirisha mchango mkubwa wa elimu ya ufundi stadi katika kutatua tatizo la ajira nchini. Aidha, VETA imefanikiwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa mafunzo ya ufundi stadi na kuwawezesha wahitimu kujiajiri.
“Kutokana na ongezeko la uwekezaji nchini, ikiwa ni pamoja na miradi ya kigeni, Serikali inaendelea na juhudi za kuongeza mafundi wenye ujuzi wa kimataifa. Takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha kuwa, kati ya Machi 2021 na Machi 2024, miradi 1,188 ilisajiliwa na kutoa ajira 345,464,”amesema CPA Kasore
Katika kuhakikisha kuwa wahitimu wanakidhi viwango vya kimataifa,Mkurugenzi huyo amesema VETA imeandaa mkakati wa kutoa mafunzo katika vituo vya umahiri nchini kote na kueleza kuwa Vituo 14 vinatarajiwa kuanzishwa ili kutoa mafunzo ya kiwango cha kimataifa, kwa lengo la kuongeza nafasi za ajira kwa wahitimu.
“VETA imepanua ushirikiano na makampuni na waajiri zaidi ya 100, kwa lengo la kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi,hii inahusisha ushirikiano na viwanda mbalimbali, ambapo wanafunzi wanapata uzoefu wa kazi katika mazingira halisi,”Kasore amesema
Ameongeza kuwa VETA imeanzisha mpango maalum wa kushirikiana na mafundi mahiri katika kutoa mafunzo ambapo unawawezesha mafundi mahiri kupata ujuzi zaidi na kurasimishwa ujuzi wao kwa kupatiwa vyeti.
“VETA inazidi kuonesha mwelekeo mzuri katika kuboresha elimu ya ufundi stadi nchini, na kuhakikisha kuwa wahitimu wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira, huku wakifanya kazi katika sekta mbalimbali na kuchangia katika uchumi wa taifa,
Juhudi hizi zinaendelea kuhakikisha kuwa VETA inakuwa chombo muhimu katika kutatua changamoto za ajira nchini”amesisitiza