Aziza Hussein, mkulima wa kijiji cha Sambwa, wilayani Kondoa, akiwaonesha wataalamu wa kilimo (hawapo pichani) hali ya shamba lake lililokauka kutokana na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Na Mwandishi Maalum
WAKULIMA katika vijiji vya wilaya za Chemba na Kondoa wamekata tamaa ya kupata mavuno ya mahindi mwaka huu kutokana na hali ya joto kali na ukame inayoendelea kukausha mashamba yao.
Aziza Hussein, (60), ni miongoni mwa waliokumbwa na athari za ukame huo baada ya shamba lake la ekari moja kukauka kabisa.
Akizungumza na Michuzi Blog kwa huzuni, Aziza anasema ametembelea shamba lake lililopo kijiji cha Sambwa, wilayani Kondoa, mkoa wa Dodoma, bila matumaini ya kupata mavuno yoyote mwaka huu.
Yeye ni miongoni mwa wakazi wengi wa kijiji hicho waliopoteza matumaini kutokana na hali mbaya ya hewa.
Kijiji chake, kama ilivyo vijiji jirani vya Keikei, Potea, Mauno na Salare, vipo katika maeneo yenye ukame, hali inayowafanya wakulima kupata mavuno kidogo kila mwaka.
Aziza anasema anakumbuka msimu wa kilimo wa mwaka 2015-2016 ambapo hawakupata mavuno yoyote….,“Naanza kuona miezi migumu mbele yetu. tukikosa mvua mwezi huu wa Machi, bei za chakula zitapanda sana na wengi hatutaweza kununua chakula,” anasema Aziza.
Anasema kwa sasa anahangaika kutafuta njia mbadala za kujipatia kipato ili aweze kuweka chakula mezani.
Katika kukabiliana na hali hiyo wakulima wa vijiji hivyo wamekuwa wakielimishwa na wataalamu wa kilimo kuhusu mbinu bora za kilimo kama mseto, uvunaji wa maji ya mvua, na upandaji wa mashimo yenye mbegu tisa ili kuhifadhi unyevu ardhini.
Hata hivyo, Aziza anasema kuwa bila mvua, mbinu zote hizo hazina msaada. Pia hawawezi kufuga mifugo kwa sababu malisho nayo hukauka.
Shirika la Inades-Formation Tanzania limekuwa likitoa mafunzo ya mbinu bora za kilimo kwa wakulima wa Chemba na Kondoa kwa miaka kadhaa sasa.
Afisa wa kilimo wa shirika hilo, Michael Kihwele, aliwashauri wakulima kutafuta vyanzo mbadala vya kipato kama ufugaji wa kuku na kutumia mbegu za muda mfupi na zinazostahimili ukame, kama vile viazi vitamu vya asili.
“Hii itawasaidia wakulima wengi kuepuka njaa kwa kuuza kuku na kununua chakula kutoka wilaya jirani,” amesema Kihwele.
Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kwa kiasi kikubwa wanawake wa vijijini, kwa sababu wao ndio wanaobeba jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa chakula, maji na kuni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.