*Wanawake hao wamzawadia jiko la umeme Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Na Mwandishi wetu.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amewataka Wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwa mabalozi kutumia nishati safi ya kupikia.
Amesema kusherekea siku ya wanawake kwa wanawake wa Tanesco bila kuwa watumiaji wa nishati safi ya kupikia haitaleta maana hivyo kutumia nishati safi ya kupikia inawezesha kuhamasisha familia na jamii kutumia nishati hiyo kwa usalama kwa afya na kwa ustawi wa vizazi vijavyo.
Dkt. Biteko ameyasema. hayo wakati wa Kongamano la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme lililiandaliwa na Wanawake wa Tanesco kuelekea maadhimisho ya Siku Wanawake Duniani ambayo hufanyika Machi 8 ya kila mwaka na kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika mkoani Arusha na Mgen Rasmi Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Katika kongamano hili nimefahamishwa kuwa limeanza kwa mjadala juu ya nafasi ya wanawake katika ajenda ya nishati safi ya kupikia ya umeme na kupitia mijadala hii tunaibua hoja muhimu na tunashirikiana na wadau wote muhimu kuweka mikakati ya kuhakikisha tunafikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” Amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amewataka kutumia fursa hiyo ya Siku ya Wanawake vyema na kuwasihi wanawake wote kuibeba ajenda hiyo muhimu ambayo Mheshimiwa Rais amekuwa akitoa kipaumbele akiwa ndani na nje ya Nchi hususan katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Ameongeza kuwa, kupitia mfuko wa Nishati safi ya kupikia, Serikali itahakikisha kuwa wanawake wanapata mikopo yenye riba nafuu ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara za nishati safi.
Pia, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Sera na Sheria mbalimbali zinakuwa rafiki kwa wawekezaji wa nishati safi ya kupikia ili waweze kushiriki kikamilifu katika biashara ya nishati safi ya kupikia.
Naye, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka watanzania hususan wanawake kuendelea kuiunga mkono ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watanzania wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo – Hanga amesema kuwa Serikali imeweka msukumo katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia nishati ya umeme kwa kuwa ni nafuu zaidi na imefika kila mahali nchini.
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Mhe. Balozi Zuhura Bundala amesema kuwa wanawake ndio wahusika wakuu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. Amesema nishati safi ya kupikia ina gharama nafuu na ni rahisi kwa matumizi.
Jukwaa hilo limelenga kuhakikisha kwamba kila Mtanzania, hususani mwanawake, anapata fursa ya kutumia nishati safi kwa kupikia.
Wanawake hao kwa kutambua umuhimu wa nishati safi ya kupikia wamempa jiko la kupikia la umeme Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko wakisema akapikie wifi yao.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko akizungumza katika Kongamano la Wanawake wa Tanesco kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani Machi 8.
Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga Akizungumza kuhusiana matumizi ya nishati safi ya kupikia na mkazo wa serikali juu ya matumizi ya nishati hiyo. Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Gissima Nyamo-Hanga akizungumza mikakati ya Tanesco katika kuhamasisha kutumia nishati ya safi ya kupikia ya umeme ,jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wanawake wa Tanesco wachereheka katika kongamano kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8.
Matukio katika picha ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko akipata maelezo katika mabanda kwenye kongamano la kuhasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme ikiwa ni kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8.