Na Mwandishi wetu, Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, kupitia mtandao wa Polisi Wanawake, limetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika Kituo cha Mafunzo kwa Watu wenye Ulemavu kilichopo wilayani Arumeru, mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Arusha (TPF NET), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Debora Lukololo, alisema msaada huo ni sehemu ya shamrashamra kuelekea Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika kitaifa mkoani Arusha. ACP Lukololo alieleza kuwa, kwa kuzingatia umuhimu wa kusaidia watu wenye uhitaji, waliona ni vyema kutoa sadaka kwa wanafunzi hao walemavu.
“Ni muhimu kutambua mahitaji ya wanafunzi hawa, kwa hiyo tumeleta vitu muhimu kwao kama magodoro, sukari, mchele, taulo za kike, na vitu vingine vya msingi ambavyo vitawezesha maisha yao kuwa bora zaidi,” alisema ACP Lukololo.
Aidha, ACP Lukololo alitoa wito kwa taasisi nyingine za kiserikali na zisizo za kiserikali kujitokeza na kuwa na utaratibu wa kuwakumbuka watu wenye uhitaji katika jamii. Alisisitiza kuwa, msaada huu hautasaidia tu watu hao bali pia utaleta baraka kutoka kwa Mungu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo hicho, Mwalimu Emmanuel Ayo, alisema kuwa Kituo cha Mafunzo kwa Watu wenye Ulemavu kilianzishwa mwaka 1988, na lengo lake kuu lilikuwa ni kuwasaidia watu wenye ulemavu kupata ujuzi utakaowasaidia kujitegemea na kuepuka kuwa tegemezi kwa familia zao. Kituo hicho hivi sasa kinawahudumia wanafunzi 214.
Wanafunzi wa Kituo hicho walionesha shukrani za dhati kwa mtandao wa Polisi Wanawake kwa msaada waliopokea, na walimwomba Mungu awabariki kwa michango yao.
Msaada huu unakuja katika kipindi muhimu ambapo jamii inahitaji kuzingatia haki za watu wenye ulemavu na kujitahidi kuwasaidia ili waweze kujitengenezea maisha bora.