Afisa Rasilimali Watu Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umeme (ETDCO) Bi. Zayana Manento (kulia) akikabidhi mahitaji ya vitu mbalimbali kwa uongozi wa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Al’hidaya kilichopo Kata ya Zingiziwa, Jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya Wanawake wa ETDCO Kuadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo Kitaifa itafanyika Machi 8, 2025 Mkoani Arusha.
Picha za matukio mbalimbali Wafanyakazi Wanawake wa Kampuni ya ETDCO wakitoa msaada wa mahitaji ya vitu mbalimbali katika Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Al’hidaya kilichopo Kata ya Zingiziwa, Dar es Salaam.
…….
Wafanyakazi Wanawake wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Umeme (ETDCO) wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutembelea Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Al’hidaya kilichopo Kata ya Zingiziwa, Jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwafariji watoto yatima kwa kuwapatia mahitaji muhimu.
Akizungumza wakati wa akikabidhi msaada, Afisa Rasilimali Watu wa ETDCO, Bi. Zayana Manento, amesema kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo waliguswa na hali ya Kituo cha Al’hidaya baada ya kutokea janga la moto lililosababisha upungufu mkubwa wa mahitaji muhimu kwa watoto na uongozi wa kituo hicho.
“Kutokana na janga la moto walilopata, Kituo cha Al’hidaya kilikumbwa na changamoto kubwa ya upungufu wa vitu muhimu, hivyo tunajivunia kuchukua hatua ya kuwasaidia ili waweze kuendelea kuishi katika mazingira bora,” amesema Bi. Manento.
Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa ETDCO, Bi. Monica Lymo, amesema kuwa lengo ni kuonyesha ushirikiano na jamii, hasa kwa watu wenye uhitaji kwa kuchangia kutatua changamoto wanazokutana nazo.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Zingiziwa, Bw. Watson Manjoro, amesema kuwa Kituo cha Al’hidaya kinahudumia watoto 82, wakiwemo 40 wa kike na 42 wa kiume, na kwamba msaada huku kutoka ETDCO umekuwa na manufaa makubwa kwa watoto hao.
Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Zingiziwa Bw. Jaffari Masanja, ametoa pongezi kwa wanawake wa ETDCO kwa kutoa msaada mkubwa, huku akieleza kuwa msaada huo umekuja wakati sahihi kutokana na janga la moto lililolikumba Kituo cha Al’hidaya.
Kwa upande wao, uongozi wa Kituo cha Watoto Yatima cha Al’hidaya wametoa shukrani za dhati kwa Kampuni ya ETDCO kwa msaada ya vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na chakula na magodoro ambayo yameimarisha hali ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu.