Na Seif Mangwangi,Arusha
KUELEKEA maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 8,2025 wadau wa michezo nchini zaidi ya 150 wanatarajiwa kushiriki kwenye kongamano la Wanawake lililoandaliwa na waandaaji wa tamasha la Tanzanite Samia women’s sports.
Kongamano hilo ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano na Baraza la Michezo la Taifa nchini, (BMT) lina lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika michezo,uongozi,na kuenzi juhudi za wanawake katika sekta ya michezo nchini.
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo ( BMT), Neema Msitha ambaye ndio mwenyekiti wa waandaaji wa tamasha hilo akiongea na waandishi wa Habari leo machi 6, 2025 jijini hapa amesema katika kongamano hilo kutakuwa na mada za kuelimisha wanawake pamoja na hadithi za mafanikio kwa wanawake waliyofanya vizuri katika tasnia ya michezo nchini.
“Nitoe mwiito kwa Wanawake wote waliopo hapa Arusha kushiriki kwa wingi kwenye kongamano hili litakaloanza kuanzia saa 3:00 asubuhi, lakini pia washiriki katika matukio muhimu yanayofanyika katika Mkoa huu ikiwemo michezo”amesema Msitha.
Msitha amesema kongamano hilo ni la nne kufanyika nchini ambapo makongamano mengine matatu yalikuwa yakifanyika Jijini Dar es saaam na kualika wanamichezo kutoka nchi jirani katika kuyanogesha.
Akizungumzia msimu wa nne wa tamasha la michezo la Tanzanite Samia Women’s Super Cup ambalo linafikia tamati leo kwa mchezo wa fainali kati ya Jkt Quuens dhidi ya Yanga Princess,mchezo ambao utapigwa kwenye uwanja wa Agha Khan uliopo Ngaramtoni amewataka wakazi wa Arusha wajitokeze kushuhudia fainali hiyo.
Amesema michezo hiyo ni maono ya Rais Samia katika kuenzi ushiriki wa Wanawake katika michezo likiwa limebaba maudhui ya kusherekea nguvu ya wanawake katika michezo “Celebrating the power of Women in Sports”.
BMT pia ilipata nafasi ya kutembelea kituo cha michezo cha Orkeeswa katika Sekondari ya Orkeeswa iliyopo wilayani Monduli na kugawa vifaa vya michezo ambapo kwa mujibu wa Msitha kituo hicho kimekuwa kikifanya vizuri kinachofanya vizuri katika kuibua na kuendeleza vipaji kwa Watoto wa Kike.