VIJANA 7, wa Ifakara mkoani Morogoro wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 28 likiwemo la kuongeza genge la uhalifu na utakatisha wa fedha zaidi ya kiasi cha Sh milioni 1.9 walizojipatia kwa njia za udanganyifu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Yonas Mwombeki (21) Godfrey Kunemba (29 ), Ramadhani Libandika (22), Amdalah Liwewa (22), Nagwa Chonja (22), Dotto Yanila (20) na Aloyce Mwelenga (22).
Washtakiwa wamesomewa mashtaka yao Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga na Wakili wa Serikali, Cathbert Mbilingi akisaidiana na Nura Manja
Akisoma hati ya mashtaka Mbilingi amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 52 la kwanza likiwa ni la kuongoza genge la uhalifu mengine yakiwa nikusambaza ujumbe usio rasmi, kutumia laini ya simu ambayo haijasajiliwa kwa jina lake, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuvuruga simu ya mkononi kwa kuwasilisha IMEI namba za simu ya mkononi aina ya Tecno T. 301 ambazo vifaa vyake viliunganishwa na Imei namba za vifaa vya simu nyingine na utakatishaji fedha.
Katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu inaidaiwa kuwa kati ya Januri Mosi, 2025 na Februari 10, 2025 mahali pasipojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania washtakiwa wote kwa pamoja waliongoza na kusimamia magenge ya uhalifu kwa lengo la kutekeleza mipango ya udanganyifu kwa njia ya kuanzisha usambazaji wa ujumbe wa kielektroniki usiotakikana na kujipatia fedha kiasi cha Sh 1,922,000 kutoka watu mbalimbali.
Katika mashtaka ya kusambaza ujumbe usiokuwa rasmi washtakiwa wote kwa nyakati tofauti kati ya Februari 2024 na Februari 2025 maeneo yasiyojulikana washtakiwa kwa nia ya kudanganya, kupitia simu za mkononi zenye namba tofauti walisambaza ujumbe usiorasmi kw watu mbali mbali.
Baadhi ya jumbe hizo zilisomeka “TCRA-M-PESA Imefungwa akaunti yako ya M-PESA kwa msaada tembelea ofisi zetu ukiwa na barua kutoka POLICE na kitambulisho chako upate msaada wa laini yako asante”
“Utaingiza iyo hela kwenye namba hii usajili ni Juma Ally Ramadhani”, “TCRA-MPESA Akaunti yako IMEFUNGWA tafadhari tembelea office zetu ukiwa na kitambulisho au namba za NIDA”.
Mashtaka mengine yalikuwa ni kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine inadaiwa kati ya 2024 na 2025 katika maeneo tofauti ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania washtakiwa walikuwa wakitumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu tofauti tofauti bila ya kutaarifu watoa huduma.
Katika shitaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inadaiwa Januari 17,2025 mahali pasipojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mshtakiwa Kunemba kupitia simu ya mkononi alijipatia Sh 45,000 kutoka kwa Albert Kwilasa kwa njia ya udanganyifu akijifanya yeye ni mwenye nyumba kwamba kodi yake imeisha anatakiwa kumtumia fedha.
Katika mashtaka ya utakatishaji fedha inadaiwa kwamba kati ya Januari Mosi, 2025 na Februari 10,2025 katika sehemu isiyojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja walijipatia Sh 1, 922,000 wakati wakijua fedha hizo ni zao tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuongoza genge la uhalifu.
Wakati huo huo washitakiwa wengine saba walipandishwa katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Kiswaga wakikabiliwa na mashitaka 24 likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kufanya utakatishaji wa kiasi cha Sh 799,401.
Weshitakiwa katika kesi hiyo ni Kelvin Sauro (25) Sadam Mugwalo (24), ELias Mkemwa (29), Sadick Chotero (30), Shafii Magwila (28) Halid Kitowelo (15) Mendard Numbeki (16) wamefikishwa mahakamani hapo.
Katika kesi hiyo washitakiwa hao walitenda makosa sawa na washitakiwa katika kesi ya awali isipokuwa katika kesi yao wanakabiliwa na shitaka la kuvuruga simu ya mkononi kwa kuwasilisha IMEI namba za simu ya mkononi aina ya Tecno T. 301 ambazo vifaa vyake viliunganishwa na Imei namba za vifaa vya simu nyingine.
Aidha, baada ya kuelezwa hayo Wakili Mbilingi alidai kuwa upelelzi wa shauri hilo bado haunakamilika na washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na kosa lao kuwa ni la uhujumu uchumi na mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa kesi inayowakabili ni ya uhujumu uchumi.
Kesi imeahirishwa hadi Machi 20, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.