*Awapongeza wananchi
kwa muitikio wa kujiunga na kuchangia ili kujiwekea akiba kwa maisha
bora ya sasa na ya baadaye kupitia kampeni ya NSSF Star Mchezo
Na MWANDISHI WETU,
Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw.
Masha Mshomba, amesema katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi
wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fursa kwa Wananchi
Waliojiajiri kujiunga na kuchangia NSSF ili wanufaike na huduma na mafao
mbalimbali yanayotolewa.
Bw. Mshomba amesema hayo tarehe 7
Machi, 2025 katika soko la Kilombero, Jijini Arusha, wakati akizungumza
na Mastaa wa Mchezo wa NSSF waliojiajiri ambao ni wakulima, wafugaji,
wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, machinga, bodaboda, wasani
mbalimbali, biashara nyingine ndogo ndogo (wasusi, wachuuzi wa masokoni,
mamalishe na baba lishe).
“Kwa muda mrefu Mastaa wa Mchezo wa
NSSF ambao ni wananchi waliojiajiri walikuwa hawanufaiki na hifadhi ya
jamii kwa kujiwekea akiba, lakini Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa
na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa nafasi kwa Wananchi
waliojiajiri kujiunga na kuchangia NSSF ili wanufaike na mafao yote
yanayotolewa pamoja na mafao la matibabu,” amesema Bw. Mshomba.
Amempongeza
Rais Mhe. Dkt. Samia kwa kutoa nafasi kwa Wananchi Waliojiajiri
kujiunga na kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya
baadaye.
Bw. Mshomba ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi
waliojiajiri kujiunga kwa wingi NSSF ili iweze kuwahifadhi wanapopata
majanga kama ya uzee, maradhi na ulemavu ambapo kwa wanaojiunga na
kuchangia NSSF itakuwa Staa wa Mchezo wa baadaye kwa kuwapa mafao na
huduma nyingine.
Amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni
kuhakikisha wananchi waliojiajiri wananufaika na hifadhi ya jamii kwa
kujiunga na kuchangia NSSF ambapo umewekwa utaratibu mzuri kwani huko
huko waliko wakibofya *152*00# wanaweza kujiunga na kuchangia kidogo
kidogo kwa siku bukubuku, kwa wiki, kwa mwezi au muhula.
Amewashukuru
Mastaa wa Mchezo wote ambao wamenufaika na elimu ya hifadhi ya jamii na
kuamua kujiunga na kuchangia kwa maisha bora ya sasa na ya baadaye.
Bw.
Mshomba amesema lengo la NSSF ni kuhakikisha wananchi waliojiajiri
popote walipo wanapata elimu ya hifadhi ya jamii, wanajiunga na
kujiwekea akiba kwani jambo hilo linaenda kuondoa umasikini nchini.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Soko la Kilombero, Bw. Rajabu Hassan,
ameishukuru
Serikali kupitia NSSF kwa kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa
Wananchi Waliojiajiri ili waweze kujiunga na kuchangia kwa ajili ya
kujenga maisha bora ya sasa na ya baadaye.
Kwa upande wake, Bw.
Gabriel Silayo, Mkurugenzi wa Uwekezaji, Mipango na Miradi,
amewahamasisha wananchi waliojiajiri kutumia fursa ya kampeni ya NSSF
Staa wa Mchezo kujiunga na kuchangia ili wanufaike na mafao yanayotolewa
na NSSF.
NSSF STAA WA MCHEZO, HIFADHI SCHEME – HIFADHI YA JAMII KWA WOTE.