Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India hapa nchini Mhe. Bishwadip Dey ofisini kwake Msalato Jijini Dodoma leo tarehe 10 Machi 2025.
Katika mazungumzo yao Jenerali Mkunda amempongeza Balozi Bishwadib Dey kwa kazi nzuri anayoifanya hapa nchini hususani kudumisha ushirikiano baina ya JWTZ na Jeshi la India katika nyanja ya Mafunzo, Mazoezi, na kubadilishana uzoefu wa kijeshi.
Aidha Mkuu wa Majeshi amemwomba Mhe Balozi kuendelea kudumisha ushirikiano baina ya Majeshi haya mawili ili kutoa fursa kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za Kijeshi.
Naye Balozi Bishwadib Dey ambaye alifika Ofisini kwa Mkuu wa Majeshi kwa ziara ya kikazi, amelishukuru JWTZ kwa ushirikiano uliopo baina ya Majeshi ya nchi hizi mbili na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo katika mafunzo, mazoezi na kubadilishana uzoefu wa Kijeshi.
Uhusiano uliopo baina ya Majeshi haya mawili ni muendelezo wa mahusiano ya muda mrefu baina ya Tanzania na India katika masuala ya Diplomasia ya Ulinzi.