WATUMISHI wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wamehimizwa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kufanikisha malengo yaliyowekwa katika mpango kazi wa taasisi hiyo.
Akizungumza na wajumbe wa baraza hilo, Dkt. Kipesha alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya idara na vitengo mbalimbali ndani ya mamlaka kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji.
Katika kikao hicho, wajumbe walipitia na kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji kutoka katika idara na vitengo vya mamlaka na kutoa maoni yao. Lengo kuu lilikuwa ni kutathmini hali halisi ya utekelezaji wa majukumu ya mamlaka na kubaini changamoto pamoja na fursa zilizopo katika kufikia malengo yake.
Aidha, wajumbe walijadili mbinu bora za kuboresha utendaji kazi wa TEA ili kuongeza tija katika sekta ya elimu. Majadiliano yalihusisha hatua zilizochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana, pamoja na mikakati ya kuimarisha mchango wa TEA katika kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia nchini.
Kwa kuzingatia umuhimu wa ushirikiano na uwajibikaji, Dkt. Kipesha aliwahimiza watumishi wote wa TEA kuendelea kujituma na kushirikiana ili kuhakikisha malengo ya mamlaka yanafikiwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu nchini.



