NA DENIS MLOWE, IRINGA,
TIMU 50 zinazotarajiwa kushiriki mashindano ya kugombea Kombe la VunjaBei lenye kitita cha sh. Milioni 10 kwa bingwa zimetakiwa kurudisha fomu leo Machi 11 ikiwa siku ya mwisho.
Akizungumza na mwanahabari Katibu wa mashindano hayo Pastor Kwambiana alisema kuwa timu zote zilizofuzu hatua ya 50 bora kwamba saa kumi jioni ya leo Machi 11 ndiyo mwisho wa dirisha la usajili na fomu za usajili zinatakiwa kufika kabla ya saa moja usiku katika kamati ya mashindano.
Kwambiana alisema kuwa kama kamati hawataongeza siku za usajili wala hawatapokea nakala fomu ya usajili baada ya muda husika kukamilika kwani wanataka kukimbizana na muda wa mashindano yaishe kama yalivyopangwa kiratiba.
Aliongeza kuwa mashindano hayo yanatarajiwa kuzinduliwa Machi 16 mwaka huu katika viwanja vya Kalenga katika ardhi ya Chifu Mkwawa kuanzia saa nne asubuhi.
Kwambiana alisema kuwa katika uznduzi huo kutakuwa na Burudani mbalimbali huku timu zote 50 zikipatiwa Vifaa kutoka kwa mdhamini wa mashindano hayo kampuni ya Vunjabei chini ya Fred Ngajilo.
Mchezo wa ufunguzi utakupigwq kwenye uwanja huo ambapo wenyeji Kalenga wanapewa nafasi kubwa kuzindua ligi hiyo kutokana na kufanyika kwenye uwanja wa nyumbani.
Alitoa wito kwa wapenzi mashabiki wa mchezo wa soka kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo kuweza kupata burudani mbalimbali zitakazojitokeza siku hiyo.