Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa, Vienna, Mhe. Naimi Sweetie Hamza Aziz amezitaka nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Dawa za Kulevya kulipa uzito unaostahili tatizo la Matumizi ya Dawa Mpya za Kulevya pamoja na Dawa tiba zenye asili ya kulevya (New Psychoactive substances NPS kwani zimekuwa tishio kwa nguvu kazi, mazingira, ustawi wa kijamii na kiuchumi, usalama wa nchi wanachama.
Tahadhari hiyo imetolewa tarehe 11 Machi, 2025 wakati Mhe. Balozi Naimi akihutubia Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Kupambana na Dawa za Kulevya unaoendelea jijini Vienna, Austria.
Pia, katika Mkutano huo, alieleza jitihada zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na mapitio ya Sera ya Taifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya 2024, na Sheria ya Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo yameweka msisitizo katika maeneo manne: kupunguza uingizwaji wa dawa za kulevya, kupunguza utegemezi, kupunguza madhara, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.
Aliuhakikishia Mkutano huo kuwa, Tanzania itaendelea kutekeleza Mikataba 3 ya Kupambana na Dawa za Kulevya na kushirikiana na nchi wanachama, jumuiya za kikanda na Umoja wa Mataifa katika jitihada za kupambana na dawa za kulevya.