Na. Leah Mabalwe, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri, awataka viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wananchi kufuata maelekezo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili kutovuruga maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Aliyasema hayo katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Dodoma kilichoketi kujadili taarifa ya mapendekezo ya mgawanyo wa Jimbo la Dodoma Mjini na kuzalisha Jimbo la Mtumba pamoja na Jimbo la Dodoma mjini. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la leo tarehe 12 Machi, 2025.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatoa fedha nyingi kwaajili ya kuboresha Mji wa Dodoma. Hivyo, napenda kuwaomba sana viongozi wangu mbalimbali wa vyama vya siasa pamoja na vijana wote kwa ujumla kuelekea katika uchaguzi mkuu wa serikali, kufuata taratibu nzuri na kuepuka vurugu, na ili kuepuka vurugu ni kufuata utaratibu mzuri wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuanzia wakati wa kujiandikisha pamoja na kuboresha taarifa katika daftari la kudumu la mpiga kura. Hivyo, inakupa haki ya kwanza ya kupiga kura kwa kujisifu kwa kuwa na kadi ya kupiga kura” alisema Alhaj Shekimweri.
Pia aliongezea kwa kuwasisitizia viongozi wote wa vyama vya siasa kutoa elimu kwa wananchi juu ya kutunza amani na umuhimu wa kupiga kura. “Kila kiongozi wa chama cha siasa anawajibu wa kutoa elimu kwa wananchi ili kulinda amani pamoja na kujitokeza katika kupiga kura. Hivyo, kila kiongozi anawajibu mkubwa sana wa kuwapa elimu wananchi wake. Nina imani kuwa haya mambo yote yakifuatwa hakutatokea na tatizo lolote la kuvuruga amani. Nawaomba sana kufuata utaratibu mzuri uliowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi’’ alisisitiza Alhaj Shekimweri.
Nae, Afisa Mtendaji wa Kata ya Hazina, Tunu Mahmoud, alipongeza zoezi hilo la ugawaji majimbo kwasababu fursa zitaongezeka na kuweka mipaka ya utawala mzuri kwa watendaji wa umma pia itarahisisha upatikanaji na utoaji wa huduma kwa ukaribu.
“Zoezi hili la ugawaji wa majimbo kati ya Jimbo la Mtumba pamoja na Jimbo la Dodoma Mjini kwa upande wangu ni jambo zuri hii itasaidia upatikanaji wa huduma wa karibu na haraka kwa wananchi. Pia itaongeza fursa za kijamii na kiuchumi pamoja na kuweka mipaka mizuri kwa watumishi wa umma. Hivyo ni jambo zuri na jiji letu la Dodoma litazidi kukua na kupata maendeleo zaidi” alisema Mahmoud.