Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini Mafuta na Gesi Asilia,Mariam Mgaya akizungumza na waandishi wa habari jijni Arusha kuhusu maandalizi ya mkutano huo .

…………..
Happy Lazaro, Arusha
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dokta Doto Mashaka Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa 62 wa bodi ya EITI utakaofanyika katika hoteli ya Gran Melia iliyopo jijiji Arusha kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo ,Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini Mafuta na Gesi Asilia,Mariam Mgaya amesema kuwa, Mkutano huo utahudhuriwa na washiriki zaidi ya mia moja ikiwa ni wajumbe wa Bodi ya EITI kutoka mataifa mbalimbali duniani ikijumuisha wawakilishi wa kampuni kubwa zinazojihusisha na shughuli za uchimbaji na utafutaji wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia, Asasi za Kiraia zinazojihusisha na shughuli za uziduaji, Sekretarieti ya EITI na wawakilishi wa nchi wanachama wa EITI duniani.
Mgaya amesema kuwa,kufanyika kwa mkutano huu hapa nchini ni fursa adhimu ya kuonesha jinsi gani nchi yetu inavyotekeleza vigezo vya kimataifa vya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia .
“kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni moja ya nchi wanachama wa EITI inayotekeleza masuala ya uwazi na uwajibikaji kisheria kupitia Sheria inayosimamia uwazi na uwajibikaji (Sheria ya uwazi na uwajibikaji katika katika rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania, 2015, SURA 447)”amesema Mgaya .
Mgaya amesema kuwa, mkutano kama huo hufanyika kwenye nchi tofauti kwani ni umoja ambao karibu nchi 57 zimejiunga na umoja huu kwa hiyo kwa mwaka huu wameamua wafanyie hapa Tanzania .
Ametaja malengo ya mkutano huo wanajadili agenda nyingi za utekelezaji na uwazi duniani na kubwa haswaa kwa mkuutano huu wanaaangalia jinsi ya kudhibiti maswala ya rushwa kwenye mnyororo mzima wa dhamani katika sekta ya uziduaji, jinsi gani watahakikisha nchi inapata rasilimali nyingi kutoka kwenye hiyo sekta ya uziduaji .
Aidha ametoa wito kwa watanzania wote kuwa Taasisi hii ni ngeni haijulikani sana ila wanatoa ripoti kila mwaka na wanazisambaza kwa wananchi wote ili wananchi waweze kushiriki katika usimamizi wa Rasilimali Madini Mafuta na Gesi asilia .
“Nawaambia Watanzania wote wasome ripoti zao na wao kama Watanzania washiriki katika kuboresha sekta ya Uziduaji ili Rasilimali ambazo tunazo ziweze kuwanufaisha wananchi wote kwa ujumla .”amesema Mgaya .