Katikati ni mkuu wa mkoa wa Rukwa Charles Makongoro Nyerere wakati akizungumza na baadhi ya viongozi alioambatana nao kwenye ukaguzi wa miradi ya maendeleo
…………………..
Na Neema Mtuka Sumbawanga,
Rukwa: Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Sumbawanga na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora na thamani ya fedha katika kila miradi.
Akiwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi leo tarehe 11, Machi 2025, Makongoro amepongeza juhudi za wataalamu na viongozi wa Manispaa kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha utoaji wa huduma katika sekta za afya ,elimu na maji.
Makongoro amewataka watendaji hao kulinda miradi hiyo pamoja na vitendea kazi ili vidumu kwa muda mrefu.
Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi wa Manispaa kuhakikisha kasi ya utekelezaji unaenda sambamba na kuzingatiwa kwa viwango vya ubora vilivyowekwa.
“Hakikisheni thamani ya fedha inayotolewa kwa ajili ya miradi inaenda sambamba na ubora wa miradi hiyo na kuitunza miundombinu hiyo,” amesema Makongoro..
Nao baadhi ya wananchi wa kata ya Sumbawanga asilia akiwemo Neema Simchondo amesema ujenzi wa kituo cha afya cha Sumbawanga asilia kitawapunguzia akina mama wajawazito na wanaonyonyesha adha ya kutembea kwenda kituo cha afya Mazwi kufata huduma.
” Ujenzi wa kituo hiki cha afya hapa Sumbawanga kumewarahisishia wananchi kupata huduma za afya kwa ukaribu zaidi.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa katika ziara hiyo ni ukamilishaji jengo la Utawala na jengo la kujifungulia katika hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga, ujenzi wa kituo cha afya Senga, kituo cha afya Sumbawanga asilia, umaliziaji wa bwalo katika Shule ya sekondari Sumbawanga na kizwite.