Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt.Batlida Burian akizungumza wakati akifungua warsha ya Mazoezi Juu ya Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kupambana na Umwagikaji wa Mafuta Kwenye Bahari na Maziwa (National Marine Oil Spill Response Contingency Plan – NMOSRCP) inayofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dk. Batilda Burian amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kuendesha mazoezi juu ya mpango wa taifa wa kujiandaa na kupambana na umwagikaji wa mafuta kwenye bahari na maziwa na kutoa vifaa vya kukabiliana na dharura kwa watu wanaofanya shughuli za kiuchumi baharini.
Mhe. Balozi Dk. Burian ametoa pongezi, leo tarehe 12 Machi, 2025, wakati akifungua warsha ya Mazoezi Juu ya Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kupambana na Umwagikaji wa Mafuta Kwenye Bahari na Maziwa (National Marine Oil Spill Response Contingency Plan – NMOSRCP) inayofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga,
Mhe. Dk. Burian amewataka wadau wa sekta hiyo kuhakikisha vifaa vya kukabiliana na dharura za umwagikaji wa mafuta vinahifadhiwa katika maeneo yanayofikika kwa urahisi na kila mmoja ili kurahisisha hatua za haraka pale dharura inapotokea ukizingatia mkoa wa Tanga ni lango la mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
“Ni lazima tujipange kikamilifu kwa kuwa Tanga inatarajiwa kuwa lango kuu la kupokea na kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima hadi Chongoleani, ambapo ujenzi wa bomba upo katika hatua za mwisho,” amesema Mhe. Balozi Dk. Burian.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira (TASAC), Wakili Leticia Mutaki kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC amesema kuwa usalama wa watu wanaofanya shughuli zao kwenye bahari na maziwa ni jambo muhimu, na TASAC imekuwa ikitoa elimu kwa wadau wote wanaohusika na shughuli hizo.
“Katika hali ya uvujaji wa mafuta, wavuvi ndio wanakuwa wa kwanza kutoa msaada wa uokozi. Ni watu tunaoshirikiana nao kupitia vyama vyao na uongozi wao hivyo, tunaweza kupata taarifa muhimu ambazo tunazitumia kuendesha operesheni za dharura,” amesema Wakili Mutaki.
Warsha hiyo ya siku tatu inawakutanisha wadau mbalimbali wanaotumia bahari na maziwa ili kujadili mikakati bora ya kujiandaa na mazoezi ya kukabiliana na umwagikaji wa mafuta, suala ambalo linaweza kuwa na athari kubwa kwa mazingira na uchumi mara dharura hiyo inapowezeka kutokea.
Matukio ya picha mbalimbali za pamoja mara baada ya kufunguliwa warsha ya Mazoezi ya Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kupambana na Umwagikaji wa Mafuta Kwenye Bahari na Maziwa (National Marine Oil Spill Response Contingency Plan – NMOSRCP) inayofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga,