Na Nihifadhi Abdulla
KATIKA jamii nyingi, wanawake wenye ulemavu wanakumbwa na changamoto nyingi zinazowazuia kushiriki katika michezo. Pamoja na uwepo wa mikataba ya kimataifa kuhusu haki za binadamu, bado kuna uelewa mdogo kuhusu nafasi ya wanawake wenye ulemavu katika sekta ya michezo.
Miongoni mwa changamoto kubwa zinazotajwa kuathiri ushiriki wao ni mitazamo potofu ya jamii juu ya Wanawake wenye ulemavu kwani mara nyingi huonekana kama wasio na uwezo wa kushiriki michezo
Tafiti na ripoti za mashirika kama UNICEF zinaonyesha kuwa ushiriki wa wanawake na wasichana wenye ulemavu kwenye michezo ni mdogo, ukifikia kati ya asilimia 10 hadi 20 pekee.
Asha Mfundo kocha wa timu ya wanawake Zanzibar anasema hiyo inachangiwa na kosefu wa miundombinu rafiki skuli pamoja na viwanja vingi vya michezo kutozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.
“Ukosefu wa elimu Kwa wazazi pia kikwazo kwani wazazi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa michezo kwa watoto wao wenye ulemavu “Amesema Mfundo
Riziki Sharif Hija, mwanafunzi mwenye ulemavu wa ngozi wa darasa la saba katika Skuli ya Kilimahewa, anaeleza kuwa anapenda mpira wa miguu, lakini skuli yake haina uwanja wa michezo. “Hili limekuwa kikwazo kikubwa kwangu kwani sina mahali pa kufanya mazoezi wala kushiriki mashindano ya michezo kama wanafunzi wengine labda kupitia clabu na Kwa wiki siku moja tu”
Pamoja na changamoto hiyo, Riziki anaamini kuwa michezo ina faida nyingi, ikiwa ni pamoja na kujenga afya ya mwili na akili pamoja na kupanua fursa za maisha, “natoa wito kwa jamii na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa watoto wenye ulemavu tunapata fursa sawa ya kushiriki michezo kwa kuimarisha miundombinu”anasema Riziki
Asha Mbwana, mzazi wa mtoto Riziki anasema kuwa jamii inapaswa kupata elimu zaidi kuhusu haki za watoto wenye ulemavu kushiriki michezo, “Mimi nimepata changamoto kutoka kwa baadhi ya wanajamii, ambao huwatenga watoto wenye ulemavu au kuwanyima fursa za kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo michezo”
“Kwa kupitia juhudi za taasisi mbalimbali zinazotetea haki za watu wenye ulemavu, Mimi binafsi nimeanza kupata mwanga kuhusu umuhimu wa kumtia moyo mtoto wangu kushiriki michezo”
Hivyo anahimiza wazazi wengine kutobagua watoto wao wenye ulemavu bali wawape nafasi sawa ya kushiriki katika shughuli zinazoweza kuwajenga kimwili na kiakili.
Taasisi mbalimbali, kwa kushirikiana na Serikali, zimeanza kutoa elimu kwa jamii ili kuongeza ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika michezo.
Hija Ramadhan kutoka Shirika la GIZ anasema katika jitihada za kutengeneza usawa wa kijinsia ni pamoja na kuhakikisha wadau wanashirikiana kuwalinda watoto na wanawake dhidi ya ukatili.
“ Lengo hili tunaweza kulifikia kwa kutumia mbinu tofauti Kwa kutoa mafunzo Kwa watu na Wadau mbalimbali kuhamashisha Michezo kwa Maendeleo,” amesema Ramadhan
Katika juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia na kuhamasisha michezo kwa maendeleo, Dkt. Mzuri Issa, Mkurugenzi wa Chama Cha waandishi wa habari wanawake TAMWA ZNZ, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuhamasisha michezo kwa wote ili kukuza ushiriki wa jinsi na hali zote katika michezo.
“Tuwe mifano mizuri ya kuwa na heshima katika jamii, kwasababu sisi tuna nafasi ya kupata mawaidha sehemu mbalimbali ya stadi za maisha. Hivyo tuna kila sababu ya kuendeleza kuimarisha na kuhamasisha michezo kwa wote,” anasema Dkt Mzuri
Afisa ustawi wa jamii, Salma kombo Abdalla, anasisitiza kuwa jamii inapaswa kubadili mitazamo hasi na badala yake iweke mazingira yanayowajenga wasichana na wanawake wenye ulemavu ili washiriki kikamilifu kwenye michezo.
“Kushiriki kwa wanawake wenye ulemavu kwenye michezo siyo tu suala la burudani bali ni haki yao ya msingi. Jamii inapaswa kubadili mitazamo, kuweka mazingira jumuishi, na kuhakikisha kuwa kila mtu anapata nafasi sawa ya kushiriki kwenye michezo,”Anasisitiza Salma