Dar es Salaam, Machi 13, 2025
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza rasmi kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Marburg (MVD) uliokuwa umethibitishwa katika Mkoa wa Kagera. Tangazo hilo limetolewa leo na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya siku 42 kupita bila kuthibitika kisa kipya cha ugonjwa huo.
Mlipuko huo ulitangazwa rasmi Januari 20, 2025, ambapo wagonjwa wawili walibainika kuwa na maambukizi na kwa masikitiko wote wawili walifariki dunia wakati wa matibabu. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilichukua hatua za haraka kudhibiti ugonjwa huo, hasa katika Halmashauri ya Biharamulo, ambako maambukizi yaliripotiwa.
Dkt. Samia amepongeza juhudi za wataalamu wa afya, maafisa ustawi wa jamii, na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa kujitoa kwao katika kukabiliana na mlipuko huo. Aidha, ametoa shukrani kwa timu ya kitaalamu inayoongozwa na Dkt. Seif Shekalaghe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, na Dkt. Grace Magembe, Mganga Mkuu wa Serikali, pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya waliowezesha kumalizika kwa mlipuko huo.
Hata hivyo, Rais ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono, kutoa taarifa za matukio yasiyo ya kawaida katika jamii, na kushirikiana na mamlaka za afya. Pia amesisitiza kuwa Tanzania bado inakabiliwa na hatari ya magonjwa mengine ya kuambukiza kama Ebola na Mpox, hivyo ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuzuia milipuko mingine.
Serikali imeahidi kuendelea kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha wananchi wake wanabaki salama dhidi ya magonjwa ya mlipuko.