Na. Leah Mabalwe, HAZINA
Diwani wa Kata ya Hazina, Samwel Mziba, amewataka wazazi pamoja na walezi kuwa kipaumbele katika maendeleo ya watoto wao shuleni.
Mziba, alisema hayo wakati wa kikao cha walimu pamoja na wazazi kilichofanyika katika Shule ya Msingi Mlezi kwa lengo la kuzungumzia maendeleo ya lishe bora kwa wanafunzi wa shule hiyo.
“Kwanza kabisa napenda kuwashukuru wazazi wote mliofika katika kikao hiki, najua mnaelewa lengo na dhumuni la kuitisha kikao hiki cha leo, tukianzia kuzungumzia suala zima la malezi kwa watoto, tunashuhudia wazazi wengi wanakuwa wametingwa sana na kazi zao, kiasi kwamba wanakua hawana muda wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni.
Hii hali si nzuri kwasabu inamjengea mtoto kufanya kila kitu anachojisikia kwa vile hakuna mtu yeyote anae weza kummfuatilia. Hivyo, basi napenda kuwahamasisha wazazi pamoja na walezi tuwe mstari wa mbele kufuatilia maendeleo ya watoto wetu shuleni’’alisema Mziba.
Pia aliongezea kwa kuwataka wazazi kujua umuhimu wa lishe bora kwa wanafunzi wawapo shuleni. “Katika masuala ya lishe bora kwa watoto ni suala muhimu sana katika Shule ya Msingi Mlezi. Kwasababu, tumeshuhudia katika shule za wenzetu mbalimbali za Jiji la Dodoma wameweka kipaumbele zaidi kwenye suala la lishe kwa kuhakikisha watototo wanapata uji pamoja na chakula cha mchana. Hii inamjengea mtoto kuwa na uelewa mzuri hata pale anapokuwa darasani.
Hivyo, basi napenda kuwasisitizia wazazi wote tuweke kipaumbele katika masuala mazima ya lishe kwa watoto wetu kwasababu mtoto hawezi kusoma vizuri hasa pale anapokuwa na njaa” aliongezea Mziba.
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mlezi, Magreth Kisanga, alimpongeza Diwani wa Kata ya Hazina kwa kuendelea kusimamia maendeleo ya wanafunzi katika shule hiyo.
“Napenda kumpongeza sana diwani wetu wa hazina kwasababu yeye amekuwa kipaumbele sana katika ufuatiliaji wa maendeleo katika shule yetu, hajatuacha nyuma kwasababu kila hatua tunayopiga ni kwasababu diwani wetu anatusaidia sana hasa katika masuala ya mbalimbali ya maendeleo ya wanafunzi wetu” alisema Kisanga.
Kwa upande wake mzazi ambae ni Edither Kishe aliwataka wazazi kujua wajibu wa maendeleo ya Watoto wao.
“Kwa upande wangu mimi kama mzazi napenda kuwaomba wazazi wenzangu kuwa mstari wa mbele zaidi kwasababu kila mzazi ni wajibu wake kufuatilia maendeleo ya mtoto wake katika maendeleo ya shule. Baadhi ya wazazi hawana uelewa kabisa kuhusiana na suala hilo la ufuatiliaji wa watoto wao, lakini katika suala zima la lishe katika shule yetu hii.
Kwa upande wangu mimi mtoto wangu huwa anakuja kunisimulia kuwa wanapata chakula kizuri na anashiba, ukikaa na mtoto na ukimjengea mtoto ukaribu atakuwa na mengi ya kukueleza” alisema Kishe.