Na Mwandishi wetu, London Uingereza.
Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake kwa uratibu taasisi ya Kili Fair inaendelea na msafara wa kunadi vivutio vya utalii katika nchi za Ulaya Magharibi ulioanza tarehe 10- 15 machi 2025 ambapo wauzaji na wanunuzi katika sekta ya utalii wanakutana katika msafara huo wenye mawakala zaidi ya 30.
Msafara huo unaojulikana kwa jina la _”My Tanzania Roadshow 2025_ ” tayari umenadi vivutio vya utalii katika miji ya Cologne Ujerumani, Antwerp Ubelgiji na Amsterdam Uholanzi ambapo kuanzia leo tarehe 13-15 Machi, 2025 msafara huo umehamia miji ya London na Manchester iliyopo nchini Uingereza kunadi vivutio vya Utalii katika soko hilo.
Akizungumzia Msafara huo, Mkurugenzi wa Masoko kutoka Bodi ya Utalii Tanzania Ernest Mwamwaja amesema, Wadau na wauzaji wa Mazao ya utalii ukihusisha vyama vya waendesha utalii, wamiliki wa hoteli, wenye kambi za kulala wageni, makampuni ya ndege kutoka Tanzania wanakutana na wanunuzi wa Utalii (Buyers) wa bara la Ulaya kwa ajili ya kufanya biashara.
Mwamwaja ameeleza kuwa Nchi za Ulaya magharibi zina idadi kubwa ya watalii wanaotembelea Tanzania ambapo takwimu za mwaka 2023 zinaonesha kuwa watalii kutoka Ujerumani ni takribani 100,000, Uingereza zaidi ya watalii 80, 000, Uholanzi watalii zaidi ya 37,000 na Ubelgiji zaidi ya watalii 17,000 wametembelea Tanzania huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kuanzia mwaka huu.
Katika Nchi wa Uingereza Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchi humo Bw. Adam Mhagama aliipongeza Kampuni ya Kili Fair kwa uratibu mzuri wa msafara wa kutangaza utalii katika nchi hiyo ambapo pia taasisi za Serikali zinatumia fursa hiyo kuelezea mazao mapya ya utalii yanayoibuliwa pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya utalii unaofanyika katika maeneo yenye vivutio ili kukidhi idadi kubwa ya wageni wanaoendelea kutembelea Tanzania
Msafara huo unaoshirikisha kampuni za Sekta binafsi zaidi ya 30 unajumuisha pia taasisi za Serikali ambazo ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) na shirika za Hifadhi za Taifa (TANAPA) ambazo ushiriki wao unatoa hakikisho kwa sekta binafsi kuwa Serikali inawaunga mkono jitihada zao kwa kuweka mazingira rafiki, kuboresha miundombinu na huduma za utalii kwa wageni wanaotembelea Tanzania.