Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAJUMBE wa kamati tendaji ya chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) wamempongeza Mwenyekiti wao Elisha Nelson Mnyawi kwa kujitolea fedha zake binafsi shilingi milioni 5.6 kwa ajili ya chama hicho.
Mwenyekiti huyo Elisha Nelson Mnyawi amejitolea fedha zake binafsi shilingi milioni 3.6 na kununua viti vitatu vipya kwa ajili ya matumizi ya ofisi ya chama hicho.
Pia Mwenyekiti huyo amejitolea fedha zake binafsi shilingi milioni 2 kwa ajili ya kulipia kodi ya pango kwa mwaka mmoja na samani za ofisi ya MAREMA Tawi la Magugu/Magara.
Mwenyekiti wa MAREMA Tawi la Nadonjukini Swalehe Abdalla akizungumza kwenye kikao cha MAREMA kilichofanyika mji mdogo wa Mirerani, amesema Mwenyekiti huyo anastahili kupongezwa kwa kujitolea kwake.
“Mnapokuwa na Mwenyekiti mwenye moyo wa kujitolea kama huyu wetu Elisha Nelson Mnyawi, inapaswa apongezwe kwani lengo ni kusaidia wachimbaji wetu kupitia chama,” amesema Swalehe.
Amesema viongozi wa chama hicho wanafanya kazi kwa kujitolea hivyo kitendo cha Mwenyekiti wao kutoa fedha zake binafsi kinapaswa kupongezwa na wachimbaji wote.
Ofisa habari na uhusiano wa MAREMA, Joseph Lyimo amempongeza Mwenyekiti huyo kwa kutimiza ahadi yake ya kuwawezesha MAREMA Tawi la Magugu/Magara samani na kuwalipia pango.
“Kutoa ahadi ni jambo moja na kutimiza ni jambo jingine, hongera sana Mwenyekiti kwa kutimiza ahadi yako uliyoitoa mara baada ya kuchaguliwa,” amesema Lyimo.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo Elisha Nelson Mnyawi amewashukuru wajumbe hao kwa kutambua vyema mchango wake katika uwezeshaji wa chama.
“Chama hiki ni chetu kwa lengo la kuhakikisha tunafikisha kero na changamoto kwa serikali kupitia vikao kwani sisi siyo wana harakati au wana siasa ni wachimbaji madini,” amesema.