Serikali imeshauriwa kuhakikisha kituo kipya cha kuhifadhi data cha taifa kinajengwa katika eneo lenye hali ya hewa ya baridi ili kupunguza gharama kubwa za umeme zinazotumika kuendesha mitambo ya kuhifadhi taarifa.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, wakati wa majumuisho ya ukaguzi wa maendeleo ya Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC) jijini Dar es Salaam.
Kakoso alisema matumizi ya umeme katika kituo hicho ni makubwa kutokana na hali ya hewa ya joto, hivyo ni muhimu kwa serikali kuzingatia eneo sahihi kabla ya kujenga kituo kipya.
“Kama hakutakuwa na ulazima wa kujenga kituo kingine Dodoma, basi muangalie sehemu nyingine yenye hali ya ubaridi ili kupunguza gharama za uendeshaji,” alisema Kakoso.
Mbali na suala la gharama za uendeshaji, kamati hiyo pia ilishauri kuwepo na kitengo maalumu cha masoko kwa ajili ya kituo hicho ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa wa serikali katika sekta ya teknolojia unaleta faida kwa taifa.
Aidha, Kakoso alisisitiza umuhimu wa taasisi zote za serikali kutumia kituo hicho kwa kuhifadhi data zao kwa sababu za kiusalama na kusaidia serikali kuongeza mapato.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Moremi Marwa, alisema tayari kampuni za serikali zaidi ya 211 na kampuni binafsi zaidi ya 80 zinatumia kituo hicho kuhifadhi data zao.
Aliongeza kuwa matumizi ya kituo hicho yanapunguza gharama za uendeshaji kwa kampuni mbalimbali kwa kuwa kinatoa huduma ya umeme wa uhakika na ulinzi wa data.
Serikali inaendelea na mikakati ya kuhakikisha taasisi zote za umma zinatumia kituo hicho ili kuimarisha usalama wa taarifa za kiserikali na kuhimiza maendeleo ya uchumi wa kidijitali.