Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini, amekabidhi vyeti kwa wahitimu wa Mafunzo ya Udereva wa Pikipiki na Bajaji, ambao aliwalipia ada katika Chuo cha VETA-Butiama ili kuwawezesha kupata ujuzi wa udereva.
Hafla hiyo fupi ya utoaji vyeti ilifanyika Machi 14, 2025, katika Ukumbi wa Kwa Mkapa Arena, Kijiji cha Nyamisisye, Kata ya Kukirango. Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sagini alisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, hivyo kusaidia kupunguza ajali.
“Awamu ya kwanza nilitoa ofa kwa watu 100, sasa hivi nahitaji 150, hivyo jumla watakuwa 250. Kundi hili litaleta mabadiliko chanya kwenye jamii katika sekta ya usafirishaji wa abiria. Nawaomba madereva wazingatie usalama kwa kuvaa kofia ngumu, kutozidisha abiria, kutofanya ‘overtake’ bila tahadhari, kutotumia mwendokasi, kuhakikisha chombo kina bima, na pia dereva awe na leseni – ambapo nitachangia gharama,” alisema Mhe. Sagini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Mara, Martine Saningo Mollel, alisema kuwa mafunzo hayo yalifanyika kuanzia Desemba 19 hadi Desemba 27, 2024, yakihusisha wanafunzi wa fani mbili za Udereva wa Bajaji na Udereva wa Pikipiki.
Aidha, alimpongeza Mbunge Sagini kwa kuridhia kufanikisha awamu nyingine ya mafunzo katika eneo hilo, kwa lengo la kuwafikia watu wengi zaidi. Alieleza kuwa ushirikiano wa chuo na Jeshi la Polisi – Kitengo cha Usalama Barabarani pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) utawezesha wahitimu kupata vyeti pamoja na leseni zao rasmi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Pikipiki Wilaya ya Butiama, Samson Otoo, aliahidi kutoa ushirikiano kwa Mbunge wa Butiama, akimsifu kwa juhudi zake za kusaidia vijana katika kata zote 18 za wilaya hiyo.