JAMES KAMALA, Afisa Habari, Nzega TC
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Mji wa Nzega kuchangamkia fursa za kiuchumi, hasa katika sekta ya huduma, kutokana na Jiografia ya kimkakati ya mji huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Kituo kipya cha Mabasi cha Nzega, ambacho kimejengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 4.3 za Kitanzania, Mhe. Majaliwa alisisitiza umuhimu wa kuwaunganisha wafanyabiashara wadogo katika mnyororo wa biashara unaokua wa mji huo.
“Natoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji na Maafisa Biashara kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanajumuishwa katika fursa za Kiuchumi ili watu wa kada zote waweze kufanya shughuli zao katika mazingira safi na yenye utaratibu mzuri,” alisema.
Waziri Mkuu alieleza kuwa Mji wa Nzega ni kitovu muhimu cha usafiri na usafirishaji, kwani mji huo ni kiunganishi muhimu kwa wasafiri wanaotoka na kuelekea mikoa mbalimbali ya Tanzania pamoja na nchi jirani.
“Kituo cha Mabasi cha Nzega ni sehemu muhimu ya kupitisha abiria wanaosafiri kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Kanda ya Ziwa, pamoja na wale wanaokwenda Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hii ni fursa kubwa ya kibiashara kwa wakazi wa Wilaya hii,” alisema.
Mh. Majaliwa aliwahimiza wafanyabiashara wa ndani kuwekeza katika shughuli za huduma muhimu kama vile chakula, vinywaji na sehemu za burudani, ambazo zinahitajika sana na wasafiri. Pia, aliishauri Halmashauri ya Mji wa Nzega kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa hoteli na nyumba za wageni kwa ajili ya wasafiri wanaohitaji malazi.
“Malori na magari mengine yanayobeba mizigo kutoka bandari za Dar es Salaam na Tanga yanahitaji sehemu za maegesho na huduma za matengenezo. Nawapongeza viongozi wa eneo hili kwa kutenga maeneo kwa shughuli hizi,” aliongeza.
Ili kusaidia wafanyabiashara kupata mitaji, Waziri Mkuu aliwahakikishia wakazi wa Nzega kuwa taasisi za kifedha ziko tayari kutoa mikopo na kuwaagiza Maafisa Biashara wa eneo hilo kusaidia kuwaunganisha wajasiriamali na taasisi za mikopo hasa mabenki.
“Serikali tayari imetenga Shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara zinazounganisha Kituo cha Mabasi cha Nzega na maeneo mengine ya mji. Hakutakiwi kuwa na vikwazo vyovyote katika biashara,” alihitimisha.