Na Mwandishi Wetu, WMTH Morogoro
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), leo Machi 14, 2025, ameshiriki zoezi la kupandisha vifaa vya ujenzi wa Mnara wa Mawasiliano katika kijiji cha Idete, Kata ya Chanzuru, Kilosa, Mkoani Morogoro.
Mnara huu ni miongoni mwa minara 758 ya Mawasiliano inayojengwa na Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, kwa lengo la kuboresha huduma za mawasiliano katika vijiji vya mbali na maeneo yenye changamoto za miundombinu.
Kati ya minara 758 inayojengwa katika maeneo mbalimbali nchini, minara 69 inajengwa katika Mkoa wa Morogoro, ambapo minara 26 ipo katika hifadhi mbalimbali na mbuga za wanyama. Kwa upande wa Wilaya ya Kilosa pekee imenufaika kwa kupata minara 17.
Aidha, kuwepo kwa mnara wa simu katika Kijiji cha Idete unaojengwa na Kampuni ya Simu ya Airtel kutasaidia kupunguza changamoto za huduma za mawasiliano katika kijiji hicho na kunufaisha wananchi zaidi ya 7,000, hivyo kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema kuwa mnara huo unatarajiwa kukamilika na kuwashwa tarehe 1 Aprili, 2025 na kukabidhiwa rasmi tarehe 15 Aprili, 2025.
Ameongeza kuwa, hadi sasa, jumla ya minara 420 kati ya 758 imekamilika na inatoa huduma. Hii ni sawa na asilimia 55 ya utekelezaji wa mradi huo.