Bahi, Dodoma.
Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Zegele – Chikopelo yenye urefu wa Km 16 sambamba na ujenzi wa Kalavati la Chikopelo kumeleta faraja kubwa kwa wananchi wa vijiji vya Chikopelo na Zegele, Wilayani Bahi, Mkoani Dodoma.
Ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kuondoa vikwazo vya barabara kupitia Mradi wa RISE unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Akizungumza kwa furaha na mwandishi wa makala haya Mwenyekiti wa Kijiji cha Chikopelo Bwawani Bw. Sumaji Mahajile Majiwa aliipongeza Serikali kwa kuwaletea Mradi huo kwani hapo awali walikuwa na changamoto kubwa ya usafiri.
“Hapo awali watoto wetu kwenda shule ya Msingi Chikopelo pamoja na wananchi kuzifikia huduma za afya katika Zahanati ya Chikopelo ambazo zipo upande wa pili wa Mto Chikopelo ilikuwa ni vigumu hasa kipindi cha masika” ameeleza
Kwa mujibu wa Bw. Mahajile, kukamilika kwa ujenzi wabarabara hiyo na na Kalavati la Chikopelo kumeleta unafuu wa usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa eneo hilo na maeneo ya jirani.
Kuhusu manufaa ya Barabara hiyo kiuchumi, amesema kuwa kitongoji chao kinajishughulisha na kilimo cha nyanya na mboga mboga hivyo kukamilika kwa barabara hiyo kutawawezesha kusafirisha mazao yao kwenda sokoni kwa wakati na gharama nafuu.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Bahi Mhandisi Respick Malya amesema kuwa Mradi huo ulikuwa na sehemu mbili ambazo ni ujenzi wa barabara ya Zegele – Chikopelo pamoja na Boksi Kalavati la Chikopelo.
Akielezea manufaa ya Mradi huo Mhandisi Malya amesema kuwa kwa kiasi kikubwa umeweza kusaidia kuwaondolea wananchi adha kubwa ya kuzifikia huduma za kijamii kama vile shule na huduma za afya.