Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, ameahidi kuchangia ujenzi wa Kanisa la Reconciliation Missionary Baptist lililopo Kigamboni, Dar es Salaam, kwa kusaidia ununuzi wa malumalu za kanisa pamoja na gypsum ili kuendeleza ujenzi wake.
Msama alitoa ahadi hiyo leo, Machi 15, 2025, alipohudhuria uzinduzi wa kanisa hilo kama mgeni rasmi. Akizungumza na waumini waliohudhuria hafla hiyo, aliwahimiza kuendelea kujitoa kwa Mungu na kuonesha mshikamano wa kiimani.
“Niwaombe ndugu zangu wa Kristo msiache kujitoa kwa Mungu. Hata mimi, kama mnavyoniona, napitia changamoto nyingi katika biashara zangu, lakini sadaka na maombi yananisaidia kuendelea kuwa imara. Nawaomba mniweke katika maombi yenu,” alisema Msama.
Ahadi yake ya kusaidia ujenzi wa kanisa hilo imepokelewa kwa shukrani na waumini, wakimtaja kama mtu mwenye moyo wa kusaidia maendeleo ya taasisi za dini.