Timu ya Mtu ni Afya ikiongozwa na Balozi Kampeni hiyo Mrisho Mpoto, na Mratibu Kitaifa Anyitike Mwitalima ikiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Godfrey Mnzava katika hafla ya Kuhitimisha ziara za Mikoani za Kampeni ya Mtu ni Afya Awamu ya Pili.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Godfrey Mnzava akizungumza katika hafla ya Kuhitimisha ziara za Mikoani za Kampeni ya Mtu ni Afya Awamu ya Pili iliyofanyika viwanja vya Mashujaa Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Balozi wa Kampeni ya Mtu ni Afya Mrisho Mpoto akipokea zawadi ya vifaa ikiwemo begi lenye vifaa mbalimbali vyenye nembo ya Mtu ni Afya, baadhi ya vifaa hivyo ni vikombe, kofia na tisheti kama ishara ya kutambua mchango wake wa kuhamasisha jamii.Zawadi hiyo ilitolewa na Mratibu wa Kampeni hiyo Anyitike Mwakitalima .Wengine ni Josephine Kapinga kutoka Wizara ya Afya pamoja Suzana Nchalla kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.
……….
Kampeni ya Mtu ni Afya awamu ya Pili imeleta mabadiliko ya tabia kwa jamii katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza katika hafla ya Kuhitimisha ziara za Mikoani za Kampeni ya Mtu ni Afya Awamu ya Pili iliyofanyika viwanja vya Mashujaa, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Godfrey Mnzava amesema kupitia Kampeni hiyo imesaidia kwa kiwango kikubwa wananchi kutambua umuhimu wa kufanya mazoezi katika kulinda Afya na kuepukana na tabia bwete.
“Kupitia Kampeni hii ya Mtu ni Afya, Fanya kweli Usibaki Nyuma, sisi watu wa Moshi tumeendelea kufanya mengi katika kulinda Afya zetu, moja ni kufanya mazoezi,usafi wa mazingira unaendelea kufanyika na Moshi tumekuwa wa pili na Mkoa wa Kilimanjaro tumekuwa wa tatu”amesema.
Katika suala la Lishe shuleni, Mkuu huyo wa Wilaya amesema pamekuwa na utaratibu wa kuwa na chakula kilichoongezewa virutubisho ili mwanafunzi awe na ufaulu mzuri darasani.
Anyitike Mwakitalima ni Mratibu wa Kampeni ya Mtu ni Afya Kitaifa kutoka Wizara ya Afya amesema kupitia Kampeni hiyo inatekeleza Afua tisa ikiwemo ujenzi na matumizi sahihi ya vyoo bora,unawaji wa mikono kwa maji tiririka na sabuni,udhibiti wa utupaji wa taka ovyo, usafishaji wa mazingira katika maeneo ya Makazi, Lishe, hedhi salama, matumizi ya nishati safi ya kupikia,maji safi na salama na umuhimu wa kufanya mazoezi.
Kwa upande wake, balozi wa Kampeni hiyo, Mrisho Mpoto amesema kupitia Kampeni hiyo imeleta mafanikio makubwa kwenye eneo la elimu ya Afya kwa Umma ambapo imesaidia ongezeko la ujenzi wa vyoo bora na kuvitumia kutoka asilimia 20 hadi asilimia 76 na kufanikisha kutokomeza ugonjwa wa Kipindupindu Mkoani Simiyu.
“Nishukuru sana Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutekeleza Kampeni hii pamoja na wananchi sasa Simiyu hakuna Kipindupindu na pia nitoe wito kwa wananchi tuendelee kuzingatia kanuni za Afya ikiwemo kufanya mazoezi Kinga ni bora kuliko tiba”amesema.
Ikumbukwe kuwa, Kampeni ya Mtu ni Afya Awamu ya Pili ilizinduliwa tarehe 9, Mei, 2024 Mkoani Pwani na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Philip Mpango na baadhi ya mambo aliyosisitiza ni kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ili kuifikia Jamii kwa haraka. na Kampeni ya Mtu ni Afya ilianza tangu mwaka 1973 ikiwa ni takribani zaidi ya miaka 50 iliyopita tangu kuanzishwa kwake