Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, ameongoza hafla fupi ya dua ya kuliombea taifa, tukio lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, serikali, na vyama vya siasa.
Viongozi mbalimbali wa dini Serikali na vyama walioshiriki katika hafla fupi ya kuliombea taifa dua
Mdau wa maendeleo Jackline Mzindakaya wakati akizungumza na baadhi ya wananchi walioshiriki katika hafla hiyo
…………….
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, amewaongoza wakazi wa mkoa huo katika dua maalum ya kumwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dua hiyo, iliyoambatana na futari, iliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na mdau wa maendeleo, Jacquiline Mzindakaya. Hafla hiyo ilifanyika Machi 15, 2025, jioni katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ikihusisha viongozi wa serikali, viongozi wa dini, wawakilishi wa vyama vya siasa, na makundi ya watu wenye mahitaji maalum.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makongoro aliwahimiza wananchi kuendelea kuliombea taifa na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo. Alimtaja Rais Samia kama kiongozi mwadilifu, msikivu, mchapakazi na mwenye uthubutu wa kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wake, Jacquiline Mzindakaya, ambaye ni mdau wa maendeleo anayeshirikiana na serikali na wadau mbalimbali katika miradi ya maendeleo mkoani Rukwa, aliwataka wananchi kutambua na kuthamini juhudi za viongozi na wadau wa maendeleo.
Baadhi ya wananchi walioshiriki, akiwemo Saumu Ramadhani, walimshukuru Mzindakaya kwa jitihada zake za kuwakutanisha na kushiriki chakula cha pamoja, jambo ambalo linaleta mshikamano na upendo katika jamii.
Mzindakaya alisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano kwa maendeleo ya mkoa na taifa, huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia watu wenye mahitaji maalum, hasa katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na mfungo wa Kwaresima.
“Kipindi hiki tukitumie kuwasaidia wenye uhitaji ili wajihisi kuwa sehemu ya jamii yetu,” alisema Mzindakaya.