OR-TAMISEMI
Serikali imeahidi kuanza ukarabati na ujenzi wa majengo ya Shule ya Msingi Kakoyoyo, ambayo ilifungwa baada ya baadhi ya majengo yake kutitia, kupata nyufa, na kuanguka kufuatia mvua kubwa zilizonyesha mapema 2024 katika Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita.
Shule hiyo, iliyojengwa kwa nguvu za wananchi mwaka 1999, ilihudumia wanafunzi 934 ambao kwa sasa wamelazimika kusoma katika Shule ya Msingi Igwamanoni kwa kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 13.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Zainab Katimba, ametembelea shule hiyo na kuthibitisha kuwa serikali itaanza ukarabati mara baada ya tathmini ya wataalamu kukamilika.
“Tumeona uhitaji mkubwa wa kurejesha shule hii, na kupitia mapato ya ndani, serikali kuu, pamoja na wadau wa maendeleo, tutahakikisha ukarabati unafanyika ili wanafunzi waendelee kusoma katika mazingira bora,” amesema.
Naye, Diwani wa Kata ya Bulega, Mhe. Erick Kagoma, ameipongeza serikali kwa hatua hiyo, akieleza kuwa kurejeshwa kwa shule hiyo kutapunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Ziara hiyo imefanyika kufuatia ombi la Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ili kuwapa wananchi taarifa kuhusu hatua za serikali katika kuboresha shule hiyo.