Na.Lusungu Helela- ROMBO
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) ni chombo muhimu kwa ustawi na maendeleo ya Taifa la Tanzania na Watu wake.
Amesema ndoto ya Tanzania ijayo haiwezi kutimia bila uwepo wa chombo hicho.
Mhe. Dkt. Mhagama ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Machi 15, 2025 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria ya kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la TAKUKURU, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro ambapo amesisitiza kuwa suala la TAKUKURU kuwa na majengo yake ya kisasa ni jambo lisiloepukika.
Amesema Kamati hiyo iliamua kuweka kipaumbele cha kuhakikisha TAKUKURU inatekeleza majukumu yake ipasavyo ambapo moja ya kipaumbele hicho ni TAKUKURU kuwa na majengo ya kisasa yatakayokuwa rafiki na wezeshi katika kusimika vifaa vya kidijitali ili kurahisisha utendaji kazi.
“Tumehakikisha TAKUKURU inakuwa na majengo ya kisasa yenye hadhi na faragha ili iweze kutimiza majukumu yake na sio majengo ya kupanga kama ilivyokuwa mwanzo amesisitiza Mhe. Dkt. Mhagama.
Amesema Kamati hiyo imeendelea kuipigania Taasisi hiyo ili iendelee kuongezewa bajeti ya fedha kila mwaka.
Kufuatia hatua hiyo Mhe. Dkt. Mhagama amesema huo ni mwelekeo wa Serikali katika kuhakikisha kuwa TAKUKURU inakuwa chombo huru, chenye uwezo wa kutenda haki kwenye Taifa.
“Sisi Wajumbe wa Kamati hii kwa pamoja tunatoa pongezi zetu za dhati kwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimama imara kwenye masuala ya rushwa katika Uongozi wake ” amesisitiza
Ameongeza kuwa “TAKUKURU mnafanya kazi yetu ya Kamati kuwa nyepesi, sisi Wanakamati tunajisikia fahari na heshima kwa jinsi mnavyowatendea Watanzania, hakika tumeridhishwa sana na utendaji wenu”
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa jengo hilo, Mhe. Dkt. Mhagama amesema Kamati yake imeridhishwa na ujenzi wa jengo hilo huku akisisitiza kuwa thamani ya fedha inaonekana dhahiri kuanzia kwenye lango kuu hadi ndani ya jengo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amesema utashi wa kisiasa wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umeiwezesha TAKUKURU kupata vitendea kazi na kutimiza majukumu yake kwenye mazingira wezeshi.
Amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita zaidi ya Watumishi 1000 wameajiriwa na TAKUKURU, ikiwa ni jitihada za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuiwezesha TAKUKURU.
Amesema mbali na magari 88 TAKUKURU iliyowezeshwa, inatarajia kwa mara nyingine tena kupokea jumla magari 100 ili kuwawezesha maafisa hao kutekeleza majukumu yao mahali popote na saa yeyote wanakohitajika.
Amesema hiyo ni nia ya dhati ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha TAKUKURU inakuwa ni chombo chenye uhalali katika jamii.
“Taasisi yetu sio tu inaziangalia Taasisi nyingine bali imekuwa mfano na kioo kwa Taasisi nyingine katika kuonesha thamani halisi ya fedha iliyotumika katika ujenzi wa jengo hili la Rombo” Mhe. Sangu amefafanua.