Na Said Mwishehe,Ileje
VIJANA
wenye sifa jitokezeni kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika
uchaguzi Mkuu mwaka huu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
Hayo
yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania
Bara Stephen Wasira alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama hicho
Wilaya ya Ileje mkoani Songwe.
Wasira amesema kwa vijana ambao
wanajiona wana uwezo na sifa za kugombea udiwani au ubunge wajipange
katika uchaguzi Mkuu ujao kwani hakuna mwenye haki miliki ya kushikilia
nafasi hizo kwa miaka mitano, isipokuwa leseni zinapatikana kupitia
kinyang’anyiro cha kushawishi wananchi na mwenye nguvu ya kushawishi
wanapata ridhaa.
Makamu Mwenyekiti Wasira alitoa Maelezo hayo
alipokuwa akiunga hoja iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa wa
Songwe Radiweli Mwapashi akiyetaka kuona vijana wapewe nafasi katika
uchaguzi huo.
Wasira amesema ili kada apate nafasi ndani ya
chama hicho lazima apambane na kukubalika kwa wananchi na kuongeza hata
wabunge na madiwani waliopo hawakugombea peke yao.
Amesema katika
uchaguzi Mkuu mwaka huu hakuna mtu kupita bila kupingwa kwahiyo hata
watakao gombea lazima walijue hilo maana wamekubaliana kijana kama
anataka kugombea muda ukifika ajitokeze na kama anataka kuwa
msindikizaji shauri yake.
Wasira amesema katika kuelekea uchaguzi
huo kwa nafasi ya udiwani na ubunge vitakuwa wazi isipokuwa nafasi ya
urais pekee ambayo tayari Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika Dodoma
umeshapitisha jina la Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea Urais.
Amesisitiza
mkutano mkuu maalum ulikubali nafasi ya Urais kugombewa na Rais Samia
Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri aliyofanya ndani ya kipindi chake
cha miaka minne ya uongozi wake.
“Tanzania inavijana wengi na
kazi ya CCM ni kujenga viongozi bora kazi waliyoifanya tangu kupata
uhuru hivyo wajitokeze wakanolewe ili wawe tayari kuwatumikia wananchi.”
Awali
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe Radiweli Mwapashi amesema vijana wengi
hasa katika mkoa huo wanaingiwa na uoga kukabiliana na madiwani na
wabunge watakaotetea nafasi hizo katika uchaguzi ujao.
Hata hivyo
amesema kuhamasisha vijana wachukue fomu isitafsiriwe kuwa anawabagua
au kuwatenga waliopo madarakani, bali anatamani kuona wanatengeneza
viongozi vijana ili Chama hicho kiendelee kupika viongozi kizazi hadi
kizazi.