Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga akizungumza na wakati wa kata wa Mang’oto Wilayani Makete Mkoani Njombe wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ya kukagua miradi ya usambazaji wa umeme, tarehe 17 Machi 2025.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Mathayo David(Katikati)akizungumza jambo wakati wakati wa ziara ya kukagua miradi ya usambazaji wa umeme katika Kata ya Mang’oto, wilayani Makete mkoani Njombe, tarehe 17 Machi 2025.Kulia ni Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga .
#Lengo ni kila Mwananchi kufahamu gharama halisi za kuunganisha umeme
#Kapinga awataka Mameneja REA, TANESCO kuongeza kasi uhamasishaji wananchi kuunganisha umeme
# Awahamasisha Wananchi kupiga namba 180 wanapopata changamoto ya umeme
NJOMBE
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeuagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kubandika gharama halisi za kuunganisha umeme na hatua za kufuata mwananchi akitaka kuunganishishiwa umeme katika Ofisi za Serikali za Vijiji ili wananchi wazifahamu kwa ufasaha kabla ya kufanya maombi.
Hayo yamesemwa tarehe 17 Machi 2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Mathayo David katika Kata ya Mang’oto, wilayani Makete mkoani Njombe wakati wa ziara ya kukagua miradi ya usambazaji wa umeme.
Mhe. Mathayo amesema ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu ya gharama halisi za kuunganisha umeme ni wakati sasa kwa TANESCO na REA kubandika katika Ofisi za Serikali za Viiji gharama husika pamoja na hatua za kufuata pindi mteja akitaka kuunganishiwa umeme.
“Wananchi wamekuwa wakizungumza tu kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme, hakuna aliyekuwa na taarifa sahihi hasa vijijini, hii inawapa hofu wanapohitaji kuunganisha umeme na pia wanapata ugumu wa kufuata huduma ofisi za TANESCO, wekeni taarifa wazi watu wazijue itaondoa mkanganyiko”, alisisitiza Mhe.Mathayo
Kwa upande wake Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amewataka REA na TANESCO kuongeza kasi ya kuwahamaisha wananchi kuungananisha umeme ikiwemo kusuka nyaya katika nyumba zao ili kuunganishiwa umeme hasa wakati miradi inapokuwa inatekelezwa katika maeneo husika ili miradi hiyo inapokamilika wananchi wengi wawe wamepata huduma ya umeme.
Aidha, amewataka wananchi kupiga simu bure katika namba 180 ambayo inatoa huduma bure kwa wateja na i kutatuliwa changamoto zao moja kwa moja na kwa haraka.
Katika ziara hiyo Wananchi wa Mang’oto wameipongeza Serikali kwa kuwapelekea umeme kwani hapo awali walikuwa wakienda Vijiji jirani kufuata huduma mbalimbali ikiwemo kusaga nafaka pamoja na chanjo katika Zahanati zenye Umeme.
Ziara hiyo pia imeshirikisha viongozi wakuu kutoka Wizara ya Nishati, akiwemo Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Khatib Kazungu, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Maafisa wengine.